KIUNGO
mkabaji na nahodha wa Simba, Jonas Mkude hivi karibuni amejikuta katika wakati
mgumu na asijue la kufanya baada ya kutofautiana na mama yake kisa timu yake
hiyo.
Inadaiwa
kuwa sababu kubwa ya hali hiyo ni kuwepo kwa taarifa kuwa Mkude tayari amesaini
mkataba wa miaka mitatu wa kuendelea kuitumikia Simba bila ya kumshirikisha
mama yake.
Mkataba
wa zamani wa Mkude ambao aliingia takriban miaka miwili iliyopita, unatarajia
kufikia tamati hivi karibuni.
Habari
za kuaminika kutoka kwa rafiki wa karibu wa Mkude ambazo gazeti hili lilizipata
zimedai kuwa baada ya mama yake kuziona taarifa hizo, alimpigia simu mwanaye
huyo na kumuuliza kwa nini kafanya hivyo bila ya kumshirikisha.
“Ilikuwa
ni balaa kwani mama yake alikuwa haelewi chochote kile alichokuwa akiambiwa Mkude
kuhusiana na suala hilo mpaka alipopata ukweli kutoka kwa mwanasheria wake
ndipo akatulia.
“Kikubwa
mama yake Mkude alichokuwa anakilalamikia ni kwamba, kwa nini asaini mkataba
bila ya kumshirikisha, wakati anapopata matatizo yeye ndiye anakuwa wa kwanza
kumshirikisha na anampatia ushauri lakini katika hili la mkataba kwa nini
kafanya kimyakimya?” kilisema chanzo hicho cha habari na kuongeza:
“Hata
hivyo, ukweli wa hilo ni kwamba Mkude hajasaini mkataba wowote na Simba mpaka
sasa ila viongozi wa timu hiyo wameamua kufanya hivyo ili kuzipoteza maboya
timu ambazo zinamhitaji na zipo katika
mazungumzo naye,” kiliongeza chanzo hicho.
Alipoulizwa
Mkude kuhusiana na suala hilo, alisema: “Siwezi kulizungumzia suala hilo ila
ninachoweza kusema ni kwamba bado naendelea kuutumikia mkataba wangu wa zamani na
Simba ambao utafikia tamati hivi karibuni.
“Kuhusu
suala la kusaini au kutosaini mkataba mpya kwa sasa siwezi kulizungumzia ila
tambua kuwa bado nautumikia mkataba wangu wa zamani ambao utafikia tamati hivi
karibuni.”
Post a Comment