LICHA ya kuifunga Yanga mabao 2-1, Kocha wa Mbeya City, Kinnah Phiri, amesisitiza kuwa timu hiyo inacheza soka la hatari zaidi kuliko Simba au Azam FC ambazo tayari amekutana nazo na zikamfunga.
Phiri aliiongoza Mbeya City kuifunga Yanga mabao 2-1, lakini kikosi hicho kilifungwa mabao 2-0 na Simba pia ilifungwa na Azam mabao 2-1, mechi zote zikichezwa kwenye Uwanja wa Sokoine.
Pamoja na kufungwa na Azam na Simba, Phiri raia wa Malawi, amesema kiufundi, Yanga ndiyo timu iliyo vizuri, kama siyo kuwahimiza vijana wake kabla ya mchezo dhidi yao, wangefungwa mabao mengi.
“Bado Yanga ndiyo timu hatari kati ya hizo. Naamini kwa soka tulilocheza dhidi ya Yanga, tungecheza vile dhidi ya Simba au Azam uhakika wa ushindi ungekuwepo, lakini wachezaji wengi walikuwa na uoga mwingi na kujikuta tunafungwa.
“Katika mchezo dhidi ya Yanga niliwahimiza kujiamini, wasiangalie majina ama ubora wa timu, badala yake wacheze kitimu zaidi na kweli tukafanikiwa, lakini ukweli ni kwamba Yanga ilitupa presha sana.
“Kipindi cha pili, (Simon) Msuva alikuwa mtu hatari zaidi,” alisema kocha huyo wa zamani wa Free States ya Afrika Kusini.

Post a Comment

 
Top