YANGA wanatarajiwa kusaka pointi tatu kwa Ruvu Shooting
katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara utakaochezwa leo kwenye
Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Akizungumzia mchezo huo, kocha mkuu wa timu hiyo, Hans van
der Pluijm, anayetarajiwa kumpisha George
Lwandamina ambaye atakuwa uwanjani baada ya kuwasili juzi usiku, alisema
hawana presha yoyote.
Mchezo huo uliopangwa kufanyika jana, ulisogezwa mbele na Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), baada ya Ruvu Shooting kuomba kutokana na uchovu wa
safari kutoka Bukoba ambako walikwenda kucheza na wenyeji Kagera Sugar, lakini
Pluijm alisema kipigo kiko palepale.
Hata hivyo, Pluijm alisema mchezo huo ni muhimu kwao
kushinda ili waweze kujiweka katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wao.
Alisema wachezaji wake wataingia uwanjani wakiwa na nguvu
mpya baada ya kuwapa nafasi ya kupumzika siku chache kabla ya mchezo huo.
“Ninahakika kesho (leo) lazima tuwafunge Ruvu Shooting kwa
idadi kubwa ya mabao, kwani kusogezwa mbele
mchezo huu kumetoa nafasi kwa wachezaji wangu kupumzika na kufanya marekebisho idara zenye upungufu,”
alisema Pluijm.
Yanga wataingia uwanjani wakitoka kuifunga Tanzania Prisons
bao 1-0 katika mchezo wa ligi hiyo, uliochezwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja
wa Sokoine jijini Mbeya.
Ruvu Shooting ambao wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu
ya kufungwa mabao 3-1 na Kagera Sugar katika mchezo wao wa mwisho uliochezwa
Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, hawatakubali
kuendelea kugawa pointi.
Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Massau Bwire, alisema kikosi
chao kipo fiti ingawa mchezo huo utakuwa mgumu kwa kuwa watakuwa ugenini.
“Hatupo tayari kuona Yanga wanachukua pointi tatu mbele
yetu, tutajitahidi ili kuwadhihirishia tuna kikosi bora chenye ushindani,”
alisema Bwire.
Bwire aliishukuru TFF kwa kulikubali ombi lao la kusogeza
mbele siku moja mchezo huo kutokana na uchovu wa safari wa wachezaji wao.
“Tulikuwa na hali mbaya, hatukupata mapumziko tumetumia muda
mwingi kusafiri kwa kutumia basi wachezaji walikuwa wamechoka, hivyo kama
tungecheza jana tungekwenda kugawa pointi na si kushindana,” alisema.
Yanga wakishinda watamaliza mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo
kwa kufikisha pointi 33 na kuendelea kushika nafasi ya pili nyuma ya Simba.
Kwa upande wao Ruvu Shooting wakishinda mchezo huo,
watapanda hadi nafasi ya tano kutoka ya saba kwa kuwa watakuwa na pointi 22.
Post a Comment