PRISONS wamekwaa kisiki baada ya Yanga kuwagomea kumtoa kwa mkopo mshambuliaji wao, Malimi Busungu, kuichezea timu hiyo katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Busungu alisajiliwa na Yanga katika msimu uliopita wa ligi hiyo akitokea Mgambo Shooting, lakini akiwa amekalishwa benchi kutokana na ushindani wa namba kutoka kwa washambuliaji wenzake, Amis Tambwe na Donald Ngoma.
Katibu Mkuu wa Prisons, Osward Morris, alisema walimhitaji Busungu kwa kipindi cha miezi sita, lakini Yanga wamewakatalia kuwapa mchezaji huyo.
Morris alisema katika barua yao ya maombi wamejibiwa kuwa mchezaji huyo bado wana mipango naye licha ya kukosa namba katika kikosi cha Hans van der Pluijm.
“Tuna tatizo la mshambuliaji katika kikosi chetu baada ya Jeremiah Juma kuwa majeruhi kwa muda mrefu, tuliwaomba Yanga watupe kwa mkopo Busungu, lakini wametujibu katika barua yetu kuwa hawawezi kutuachia kwa sababu wana mipango naye,” alisema Morris.
Morris alisema wanaendelea kusaka mshambuliaji ambaye ataweza kuziba pengo la Jeremiah anayeuguza jeraha la goti.
Prisons inashika nafasi ya saba kutokana na pointi 19, baada ya kushinda michezo minne ikitoka sare mara saba na kupoteza minne.
Simba wanaongoza katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kufikisha pointi 35 ikishinda michezo 11 huku ikitoka sare mbili na kufungwa miwili na Yanga wanashika nafasi ya pili kutokana na pointi 33, walioshinda michezo10 sare tatu na kufungwa miwili.
Post a Comment