NAHODHA wa Yanga, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima,
ametoa neno la heshima kwa kocha wao anayeondoka, Hans van Der Pluijm, raia wa
Uholanzi, kwa kusema anapaswa kupewa heshima zote kwa jinsi alivyowaongoza
katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.
Niyonzima ameyasema hayo siku chache baada ya
Yanga kumpa mkataba wa miaka miwili, Mzambia, George Lwandamina ambaye anachukua
mikoba ya Mholanzi huyo, ingawa uongozi unawazunga wanachama kwa kukana.
Mnyarwanda huyo amesema ugumu walioupitia katika
mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, bila ya uwepo wa Pluijm hajui kama
wangefanikiwa kuwa nafasi ya pili waliyopo sasa nyuma ya Simba.
“Haikuwa rahisi kwa sisi kumaliza mzunguko huu
tukiwa hapa kwani hakuna aliyetarajia kama tungeweza kupambana kwa jinsi
tulivyokuwa tumechoka, lakini tunamshukuru Mungu kwa kutupigania.
“Yaani kama asingekuwa Pluijm na benchi zima la
ufundi kwa jinsi walivyokuwa wakitupa moyo wa kupambana na kutuambia tusikate
tamaa, sidhani kama tungefanikiwa.
“Niseme tu, nimeamini kwamba katika dunia hii
lolote linawezekana, hivyo tunaamini kwamba mzunguko wa pili tutafanya vizuri
zaidi ya hapa,” alisema Niyonzima.
Yanga imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa nafasi
ya pili baada ya kujikusanyia pointi 33, nyuma ya vinara Simba wanaoongoza ligi
hiyo kwa pointi 35.
Hata hivyo, Niyonzima alisema kuondoka kwa Pluijm
na kuja Lwandamina wao kama wachezaji hawana la kusema zaidi ya kuendelea
kushirikiana naye ili tu kuubakisha ubingwa Yanga kwa mara ya tatu mfululizo
kwani hakuna timu itakayozuia hilo.
"Tutafanya kazi na kocha yeyote yule
atakayekuja, lakini kwa sasa niseme tu Simba wapo kwenye nafasi yetu na hilo
linajulikana, wao wamekaa tu pale kwa muda, mzunguko wa pili lazima watuachie
na tuwe mabingwa. Mzunguko wa pili uwezo wetu utaongezeka maradufu na tutacheza
kufa na kupona,” alisema Niyonzima.
Post a Comment