Lwandamina anasubiri ripoti ya Pluijm aanze kazi
HUKU dirisha dogo la usajili likiwa limefunguliwa juzi, kocha mpya wa Yanga, Mzambia Goerge Lwandamina, anatarajiwa kufanya usajili kulingana na mapendekezo ya ripoti atakayokabidhiwa na mtangulizi wake, Hans van der Pluijm.
Lwandamina anatarajiwa kupokea ripoti kutoka kwa Pluijm wakati wowote kuanzia sasa, ripoti ambayo ataifanyia kazi baada ya wachezaji kurejea kutoka kwenye mapumziko.
Ripoti hiyo pamoja na mambo mengine, itakuwa imeainisha mapungufu yaliyojitokeza kwenye michuano ya kimataifa iliyoshiriki timu hiyo na ile ya Ligi Kuu Tanzania Bara mzunguko wa kwanza.
Kwa mujibu wa kigogo mmoja kutoka ndani ya timu hiyo, aliliambia BINGWA kuwa, katika ripoti ya awali ya Pluijm iliainisha mahitaji ya kiungo mkabaji, beki wa kushoto na straika.
“Kocha Lwandamina amekuwa akiifuatilia kwa karibu sana timu kupitia mikanda ya video kuanzia michuano ya kimataifa, ameshauri akutane na wachezaji wote awaone, lakini pia apitie ripoti ya Pluijm na benchi lake pamoja na kukaa nao wote kama itawezekana kisha washauriane namna ya kujenga kikosi imara,” alisema mtoa habari wetu.
“Kwanza kocha kasema timu inawapiga vichwa wawili tu ambao ni Andrew Vicent (Dante) na Vicent Bossou kwa hiyo anahitaji kiungo mmoja mkabaji ambaye naye pia atakuwa na uwezo mkubwa kupiga mipira ya vichwa na si kukaba tu ili aweze kuwa na timu bora,” alisema.
Kocha huyo yupo nchini kwa wiki moja akiwa amefichwa kwenye moja ya hoteli kubwa hapa nchini na bado Yanga haijaweka wazi ujio wake wala kuamua kutangaza jambo lolote kuhusiana na benchi lake ya ufundi.
Post a Comment