UONGOZI wa Klabu
Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, unayofuraha kuwaataarifu wapenzi wa
soka kuwa jioni ya leo umefanikiwa kuingia mkataba wa miaka mitatu na kiungo
mshambuliaji kutoka Ghana, Enock Atta Agyei.
Agosti mwaka huu, Azam FC tuliingia makubaliano maalumu na
Medeama ya Ghana juu ya kumsajili kinda huyo anayetimiza umri wa miaka 18
mwakani baada ya benchi la ufundi kuridhishwa na uwezo wake na sasa amejiunga
rasmi kwenye viunga vya Azam Complex.
Agyei anasaini mkataba tayari kabisa kuanza kuitumikia Azam
FC katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) mwakani
pamoja na michuano mingine ikiwemo Kombe la Shirikisho Afrika.
Tunaamini ya kuwa ujio wa nyota huyo wa timu ya Taifa ya
Vijana ya Ghana chini ya miaka 17, utazidi kuipa nguvu timu yetu kuelekea
kwenye michuano inayotukabili mbeleni, hivyo tunapenda kumtakia mafanikio mema
kwa kipindi chote atakachokuwa akiipigania jezi ya Azam FC.
Azam FC tunapenda kuwafahamisha mashabiki wetu kuwa
tutaendelea kukifanyia marekebisho kikosi chetu kuelekea usajili wa dirisha
dogo, lengo ni kukipa nguvu kikosi hicho ili kifanye vizuri zaidi katika
michuano ya hapa nchini pamoja na ile ya Kimataifa.
Lengo kubwa la Azam FC ni kuendelea kuwafurahisha mashabiki
wetu kwa kupata matokeo bora uwanjani, na tunaamini ya kuwa, benchi zuri la
ufundi tulilokuwa nalo, wachezaji wazuri walioko kikosini na wengine
watakaokuja kuongeza nguvu, wote kwa pamoja wataweza kutuvusha kuelekea safari
ya mafanikio msimu huu.
Hivyo, tunawaomba mashabiki wetu kuvuta subira na kuendelea
kuisapoti timu kwani tunaamini ya kuwa nyie ndio nguzo muhimu ya 12 uwanjani
katika kuwapa hamasa wachezaji ya kupata matokeo bora pamoja na kuijenga timu
kiujumla.
Wakati huo huo, leo tumewapokea wachezaji saba waliokuja
kwenye majaribio ya kujiunga na Azam FC, ambao ni mabeki wa kati Mbimbe Aaron
Nkot (Cameroon), Kone Nabil Ibrahim (Ivory Coast), kiungo mkabaji Kingue Mpondo
Stephane (Cameroon),
Wengine ni washambuliaji Yaya Awaba Joel (Cameroon), Samuel
Afful, Benard Ofori (wote Ghana) na Konan Oussou kutoka Ivory Coast.
Post a Comment