KIUNGO mchezeshaji wa Simba, Mzamiru Yassin, ameweka rekodi ya aina yake msimu huu wa Ligi Kuu Bara kwa kuweza kuwafunika viungo wote.

Rekodi hiyo aliyoiweka kiungo huyo ni ya kuwazidi viungo wote tegemeo wa timu zinazoshiriki ligi kuu msimu huu kwa idadi ya mabao aliyofikisha (manne) sawa na kiungo wa Mbeya City, Rafael Alpha.

Kati ya viungo nyota na tegemeo waliopotezwa ni Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, Thabani Kamusoko (Zimbabwe) wote wa Yanga na Salum Abubakary ‘Sure Boy’ (Azam).

Wengine ni Jean Baptiste Mugiraneza (Rwanda) ambaye hajafunga bao huku Mohammed Ibrahim (Simba) akiwa na mabao mawili wakati Frank Domayo na Mudathiri Yahaya wote wa Azam FC wakifunga kila mmoja bao moja.

Mzamiru alitua kuichezea timu hiyo msimu huu wa ligi kuu akitokea Mtibwa Sugar akisaini mkataba kwa dau la shilingi milioni 25.

Akizungumzia hilo, Mzamiru alisema mabao hayo anayofunga yanatokana na umoja na ushirikiano ambao anaupata kutoka kwa wachezaji wake.

“Moja ya vitu ninavyofurahia tangu nimetua kuichezea Simba, ni umoja na ushirikiano ninaoupata kutoka kwa wachezaji wenzangu, kama unavyojua mimi huu ndiyo msimu wangu wa kwanza.

“Hivyo, ninafurahia haya mafanikio ninayoyapata na kuahidi kuendelea kufunga na kutengeneza nafasi za kufunga mabao kwa kila nafasi nitakayoipata, ninaamini hilo litawezekana kutokana na ushirikiano uliopo kwenye timu,” alisema Mzamiru.


Post a Comment

 
Top