WAKATI Simba wakiamini kuwa beki wao wa zamani, Hassan Isihaka si lolote, nyota huyo amepata dili nchini Marekani katika Klabu ya Seattle Sounders ambapo huenda wiki ijayo akatimka zake.
Taarifa hizo za Isihaka kutimkia nchini humo zilitoka katika mtandao wa Klabu hiyo ya nchini Marekani, ambao ulimnukuu Mkurugenzi wa African Lyon, Raheem Kangenzi ‘Zamunda’ akisema mbali na beki huyo, pia kipa Rostand Youthe.
Taarifa hiyo ilikwenda mbali zaidi na kudai kuwa huenda Isihaka asionekane mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwani mambo yakienda sawa muda huo atakuwa anakula zake bata Marekani.
Baada ya DIMBA kuzinasa taarifa hizo, lilimtafuta Mkurugenzi huyo ambaye alithibitisha kuwa ni kweli Isihaka amepata dili hilo pamoja na kipa huyo na kwamba muda wowote wataondoka nchini.
“Hizo taarifa ni za kweli kabisa, kama mambo yakienda sawa ndani ya siku chache zijazo Isihaka atakwenda Marekani katika Klabu hiyo na kuhusu kipa wetu naye amepata ofa hiyo, lakini pia ipo ofa nyingine kutoka China, hivyo tunasubiri kuona ni wapi patafaa zaidi,” alisema Zamunda.
Isihaka anacheza African Lyon kwa mkopo, huku timu hiyo ikiwa ya kwanza kuifunga Simba kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kwa bao 1-0, mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

 
Top