TIMU za Ligi Kuu Bara zipo mbio kuhakikisha zinafanya usajili makini kwa timu zao, sasa beki wa kati wa Yanga, Vincent Bossou yupo kwao Togo katika mapumziko, akiwa huko ametuma dongo kwa timu pinzani.
Bossou ambaye Januari mwakani atacheza mechi za nchi yake za Kombe la Mataifa ya Afrika huko Gabon, amesema hata wapinzani wao wasajili wachezaji wa aina gani atapambana nao wasimpe tabu.
Simba inatajwa kuwa katika harakati za kumrejesha mshambuliaji wake wa zamani Emmanuel Okwi huku Azam FC ikiwa imeshawasajili washambuliaji Samuel Afful, Enock Atta Agyei na Yahaya Mohammed.
Simba inaongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 35 kileleni ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 33, Azam ni ya tatu ikiwa na pointi 25, hivyo ni wazi Yanga inawania ubingwa na timu hizo mbili.
Akizungumza na Championi Jumamosi kutoka Togo, Bossou alisema anafahamu kwamba mzunguko wa pili wa ligi kila timu itakuwa imepania, hivyo anajiandaa kukabiliana na changamoto zozote atakazokutana nazo.
“Najua timu zinafanya usajili huko, mimi huku najiandaa kupambana na hali yoyote nitakayokutana nayo kutoka timu zilizosajili wachezaji wapya ndiyo maana nafanya mazoezi ya nguvu huku.
“Nataka wapinzani wetu uwanjani wasiweze kufanikiwa hata kama wamebadili vikosi vyao, naamini bado Yanga ina nafasi ya kutetea ubingwa wake,” alisema Bossou.

Post a Comment

 
Top