Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF), limemteua
Jonesia Rukyaaa - Mwamuzi wa soka kutoka Tanzania kuwa miongoni mwa waamuzi wa
kati 10 watakaochezesha mechi za Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa
wanawake zitakazofanyika kwa wiki mbili kuanzia Novemba 19, mwaka huu.
Kwa uteuzi huo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), amempigia simu Jonesia kumpongeza kwa hatua hiyo ambayo ni
sehemu kubwa ya mafanikio ya soka la Tanzania kufanya vema katika medani za
kimataifa.
Rais Malinzi amesema kwamba Mwamuzi Jonesia ameliletea
heshima taifa la Tanzania kwa kujijengea heshima ya kuaminika mbele ya Kamati
ya Ufundi ya CAF – Waratibu na Waandaaji wa fainali hizo zitakazofanyika
Cemaroon ambako mechi za mechi ya mwisho ya fainali itafanyika Desemba 3, mwaka
huu.
“Namtakia kila la kheri, naamini kwamba Jonesia atafanya
vema. Nina uhakika kwamba hii ndiyo njia yake pekee ya kufanikiwa zaidi kwani
ipo siku atateuliwa kuchezesha hata fainali za Kombe la Dunia,” yalikuwa ni
maneno ya Malinzi akimwelezea Jonesia kwenye simu leo mchana.
Jonesia anafanya idadi ya waamuzi watakaochezesha mchezo huo
kutoka nchi za Afrika Mashariki kuwa watano kwani wengine kwa mujibu wa orodha
ya CAF ni Salma Mukansanga (Rwanda),
Lydia Tafesse (Ethiopia), Carolyne Wanjala (Kenya) na Suan Ratunga (Burundi).
Waamuzi wengine ni Maria Packuita wa Mauritius, Gladys
Lengwe (Zambia), Akhona Zennith Makalima (Afrika Kusini), Jeanne Ekoumou
(Cameroon) na Aissata Amegee (Togo). Katika orodha hiyo pia yumo Mary Njoroge wa
Kenya ambaye mwamuzi wa pembeni pekee.
Katika fainali hizo, timu shiriki ni Cameroon, Afrika
Kusini, Misri na Zimbabwe zipo kundi A wakati Nigeria, Ghana, Kenya na Mali
zimo kundi B.
Jonesia ambaye jana Jumanne alirejea kutoka Cameroon kwenye
kozi ya uamuzi ngazi ya juu, kesho Alhamisi anatarajiwa kuwa mwamuzi wa kati
kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pale Mtibwa Sugar ya
Morogoro itakapokaribishwa na Mwadui kwenye Uwanja wa Mwadui. Mchezo mwingine
utakuwa ni kati ya Mbao Fc na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini
Mwanza.
Post a Comment