LICHA ya kwamba Yanga leo Jumatatu inaanza rasmi
kambi yake ya kujiwinda na mzunguko wa pili wa ligi, beki wa kikosi hicho,
Mtogo, Vincent Bossou, hatakuwepo katika kambi hiyo kutokana na kuelekea nchini
Vietnam.
Bossou ambaye anaunda safu ngumu ya ulinzi ya
timu hiyo akishirikiana kwa ukaribu na Kelvin Yondani na Andrew Vicent ‘Dante’,
wameweza kuisaidia timu hiyo kumaliza katika nafasi ya pili katika msimamo wa
ligi ikiwa na pointi 33 nyuma ya Simba yenye 35.
Leo Yanga inaanza mazoezi kwa mara ya kwanza
ikiwa chini ya kocha Mzambia, George Lwandamina baada ya Mholanzi, Hans van Der
Pluijm kubadilishiwa majukumu, akipelekwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi klabuni
hapo.
Hata hivyo, Bossou hatakuwepo katika mazoezi hayo
chini ya Lwandamina.
Bossou ameweka bayana kwamba atachelewa kujiunga
na wenzake Jumatatu kutokana na kumpeleka ndugu yake nchini Vietnam kusaini
mkataba na moja ya timu za nchini humo ambapo atatua hapa nchini Desemba 3.
“Mimi nitarudi nchini Desemba 3, siku sita baada
ya kambi kwa ajili ya kujiunga na wenzangu pamoja na kocha mpya George
Lwandamina, nitakosekana kwa siku hizo kwa sababu nitasafiri kuelekea nchini
Vietnam.
“Naenda kumsindikiza ndugu yangu kusaini mkataba
na moja ya timu za huko pamoja na mimi mwenyewe kumalizana na timu ambayo
nitaenda kujiunga nayo baada ya mkataba wangu kumalizika hapa Yanga,” alisema
Bossou anayetarajiwa kumaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu.
Post a Comment