KOCHA mpya wa Yanga, George Lwandamina, anatarajiwa kutua
nchini leo na atasaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia timu hiyo, huku
akilipwa mshahara wa Sh milioni 40 kwa mwezi.
Mshahara huo atakaokuwa analipwa kwenye klabu ya Yanga
unauzidi ule aliokuwa analipwa kwenye timu yake ya zamani ambao ulikuwa ni dola
4,000 sawa na shilingi milioni 8.8.
Lwandamina aliyekuwa anaifundisha Zesco United ya Zambia,
amesaini mkataba huo Novemba 9 mwaka huu, tayari amejiuzulu kuifundisha timu
hiyo baada ya mpango wake wa kuhamia Yanga kukamilika.
Kocha huyo anatarajiwa kuanza kazi ya kuinoa Yanga kwenye
mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara utakaoanza Desemba 17, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, Lwandamina anatarajiwa kutua
nchini leo akitokea Zambia baada ya kumalizana na uongozi wa Zesco na kuwaaga
wachezaji wake.
Kocha huyo anakuja kuchukua nafasi ya kocha wa sasa wa
Wanajangwani hao, Hans van der Pluijm ambaye uongozi upo kwenye mpango wa
kumbadilishia majukumu na kuwa Mkurugenzi wa benchi la ufundi.
Baada ya kuwasili nchini, Lwandamina anatarajiwa kuishuhudia
Yanga akiwa jukwaani wakati wakicheza mechi yao ya mwisho kwenye mzunguko wa
kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting, mchezo unaotarajiwa kupigwa
kesho kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Post a Comment