WINGA wa Kimataifa wa Yanga, Simon Msuva, hatimaye ameeleza ukweli kuhusu suala lake na klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, ambalo limekuwa likimtafuna kwa miaka yote anapoitumikia klabu yake ya Yanga.
Msuva ambaye ni mfungaji na mchezaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2014/2015, amesema, licha ya shutuma zote anazotupiwa na mashabiki wa Yanga, bado ana maisha yenye furaha ndani ya kikosi hicho cha Jangwani.
Alisema suala la yeye kuwa shabiki wa Simba, halina ukweli wowote na kwamba yeye binafsi alikuwa shabiki wa mshambuliaji wa timu hiyo ambaye kwa sasa ni Meneja wa timu hiyo, Mussa Hassan ‘Mgosi’ ambaye ndiye alikuwa akimfanya kwenda kuangalia mazoezi na hata mechi za Simba.
“Mimi ‘role model’ wangu ni Mgosi, mara zote nilikuwa nakwenda Simba kwa ajili yake, nimejifunza mengi sana kwake na yeye ndiye aliyenipa jezi yake ambayo mashabiki wengi wa Yanga wanailalamikia hadi hivi leo,” alisema.
Alisema kwa sasa bado ana makataba mrefu na klabu yake ya Yanga na hawezi kufanya mazungumzo yoyote na klabu nyingine kutokana na kubanwa na mkataba huo.
“Kwanza sina mpango wa kucheza zaidi ligi ya nyumbani, unajua kama mchezaji nina malengo yangu na nimepanga kucheza nje ya nchi ambako ninaamini viongozi wa timu yangu wamekuwa na mipango kadhaa ya kuhakikisha kwamba natoka timu ya nje muda si mrefu,” alisema.
Alisema kuna ofa nyingi za klabu mbalimbali za nje ya nchi ambazo zinahitaji huduma yake kwa sasa, lakini bado kuna masuala yanafanyiwa kazi na uongozi wake na kwamba hawezi kuzitaja timu hiyo kwa sababu suala hilo liko nje ya uwezo wake kwa sasa.
Post a Comment