JONAS Mkude amesema klabu yoyote ikimfuata kwa
ajili ya kumsajili, ikiwemo Yanga, haraka atakwenda kumwaga wino, kwani Simba
hivi sasa inamzingua tu.
Mkude ametoa kauli hiyo akizungumza na waandishi
wetu wikiendi iliyopita, ukiwa ni muda mfupi baada ya taarifa kuibuka kuwa
mfanyabiashara maarufu hapa nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ alimwaga fedha Msimbazi
kuhakikisha kiungo huyo na fowadi Ibrahim Ajibu wanasaini mikataba mipya.
Wachezaji wao ambao Simba imewalea kwa muda mrefu
kuanzia kikosi cha vijana, mikataba yao inamalizika mwezi Januari na Mei
mwakani.
Mkude ambaye mkataba wake na Simba unafikia
tamati mwezi Januari, mwakani, alisema mpaka sasa haelewi chochote kama
ataendelea kuitumikia timu hiyo au la.
Alisema mpaka sasa hajafanya mazungumzo yoyote na
uongozi wa timu hiyo na umekuwa ukimzungusha mara kwa mara jambo ambalo
limemfanya aone kuwa hahitajiki ndani ya kikosi hicho, hivyo amewataka Yanga
wakamsajili kama kweli wanamhitaji na akasisitiza kuwa yeye yupo tayari
kujiunga na timu hiyo.
Mkude alisema viongozi wa Simba wamemzingua zaidi
baada ya kutangaza kuwa tayari ameshasaini mkataba wakati siyo kweli.
“Jamaa siwaelewi kabisa, naona wananichukulia poa
kwani wamekuwa wakinizungusha kuhusiana na mkataba mpya kila ninapowauliza,
matokeo yake wakaamua kuniharibia kuwa nimeishasaini tayari, jambo ambalo si
kweli.
“Soka ndiyo maisha yangu, hivyo kutokana na hali
hii, nipo tayari kujiunga na timu yoyote ile ambayo itanihitaji, kama Yanga
wapo tayari kunisajili mimi sina tatizo waje tu, tuzungumze na tukikubaliana
nitajiunga nao. Ninaangalia Maslahi ili kuboresha maisha yangu. Hapa nilipo
namsubiri mtu wangu mmoja amesafiri anarudi kesho (leo Jumatatu), ili tuangalie
kama nitamwaga wino Simba au sehemu nyingine,” alisema Mkude ambaye pia ni
nahodha wa Simba.
Hata hivyo, habari za kuaminika kutoka ndani ya
Simba ambazo gazeti hili lilizipata jana, zilidai kuwa uongozi wa timu hiyo
ulikuwa ukutane na Mkude, Ijumaa iliyopita kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo
la mkataba mpya.
Lakini mazungumzo hayo yaligonga mwamba baada ya
Mkude kutotokea na alipopigiwa simu alidai kuwa safarini Morogoro, hivyo
asingeweza kufika kwa wakati, hivyo watafute siku nyingine.
“Ukweli ni
kwamba siku hiyo hakuwa Morogoro, bali alikuwa nyumbani na mimi nilikuwa naye
ila aliamua kutokwenda kukutana na viongozi hao kwa kile alichodai kuwa
wanaonyesha dharau dhidi yake, hivyo hawezi kuonana nao mpaka awe na
mwanasheria wake ambaye siku hiyo hakuwepo Dar es Salaam.
“Hata hivyo, viongozi wa Simba wanatakiwa kuwa
makini kama kweli bado wanamhitaji Mkude katika kikosi chao, vinginevyo ikifika
mwezi Januari hawajamalizana naye anaweza kutimka kwani Yanga wanamsumbua kila
siku ila yeye amekuwa akiogopa kuwa watu watamuonaje kama atajiunga na timu
hiyo na kuiacha ile ambayo imeibua kipaji chake,” kilisema chanzo hicho cha
habari.
Post a Comment