UONGOZI wa Klabu ya Simba, umefikia
makubaliano na beki wake, Mohamed Zimbwe Jr ambaye ni maarufu kama Tshabalala.
Hivi karibuni kumekuwa na taarifa
kwamba Zimbwe ana mpango wa kujiunga na Yanga kwa kuwa mkataba wake na Simba
umeisha.
Championi Ijumaa, jana lilimshuhudia
beki huyo akitua kwenye ofisi za Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba,
Zacharia Hans Poppe akiwa ameongozana na meneja wake, Herry Mzozo.
Mazungumzo yao yalichukua kama dakika
25, baadaye Zimbwe Jr alitoka nje na baba yake alitoka nje kabla ya kurejea
tena ndani na kumalizana.
Baada ya mazungumzo hayo, Hans Poppe
alisema walikuwa wamemalizana kwa maana ya makubaliano na kila kitu.
“Sasa tumemalizana na Tshabalala,
awali tulizungumza na leo ilikuwa ni kumalizia tu,” alisema Hans Poppe.
Mzozo naye alithibitisha kuhusiana na
hilo: “Kweli tumemalizana kwa maana ya nini kifanyike, suala la maslahi na kila
kitu. Hapa kilichobaki ni suala moja tu, kusainishana mikataba.”
Baada ya suala la beki huyo wa
kushoto, sasa ni suala la kiungo Jonas Mkude ambaye pia amekuwa akielezwa
kwamba ana mpango wa kujiunga na Yanga, hata hivyo, Kamati ya Utendaji ya Simba
inakutana leo Ijumaa kwa ajili ya kujadili masuala kadhaa lakini la usajili
linaonekana kuwa namba moja.
Post a Comment