WAKATI suala la beki Hassan Kessy kusajiliwa Yanga akitokea Simba likiendelea kuwaumiza Wanasimba kiasi cha kutishia kwenda kushtaki katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), jingine limeibuka ambalo linawapasua kichwa kwa sasa.

Uongozi wa Simba umesema utalazimikia kufika kwenye mamlaka ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) iwapo Chama cha Soka cha DR Congo (Fecofa), hakitatoa kwa muda Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC), za wachezaji wao, Besala Bokungu na Mousa Ndusha.

Wachezaji hao wameendelea kuishia kufanya mazoezi, jambo ambalo wanasema linawaathiri wao binafsi na timu yao kwa jumla.

Wakongo hao ndiyo wachezaji pekee kati ya watano waliosajiliwa kwenye dirisha kubwa la msimu huu ambao wameendelea kutocheza kutokana na kukosekana kwa ITC, hivyo Simba imesema inatoa siku 14 tu kwa Fecofa, tofauti na hapo watawasilisha mashtaka yao Fifa.

Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele ameliambia Championi Ijumaa kuwa hakuna sababu ya msingi inayotolewa na chama hicho zaidi ya longolongo.

“Hakuna jibu la maana, ni longolongo tu lakini hakuna kikwazo chochote zaidi ya kujichelewesha tu. Tumeshaomba sana lakini kimya kimetawala,” alisema Kahemele na kuendelea:

“Kwa sasa tunaendeleza mawasiliano, sisi hatutaki kukwaruzana maana kesho keshokutwa tunaweza kutaka mchezaji mwingine huko kwao, lakini ukimya ukiendelea tutakuwa hatuna jinsi zaidi ya kuchukua hatua ili kutafuta haki yetu.”

Tofauti na Wakongo hao, Kocha wa Simba, Joseph Omog ameshawatumia nyota wapya Laudit Mavugo (Burundi), Fredric Blagnon (Ivory Coast) na Method Mwanjale raia wa Zimbambwe.

Post a Comment

 
Top