VITA ya kuidhamini klabu ya Yanga inazidi kunoga baada ya kampuni zaidi ya 20 kujitokeza kwenye kikao maalumu cha kujadili udhamini mpya wa klabu hiyo ya Jangwani.
Katika kikao hicho cha saa nne kilichofanyika Septemba 1, mwaka huu katika Hoteli ya Double Tree ya jijini Dar es Salaam, wadau kutoka kampuni mbalimbali nchini walijitokeza kuchangamkia fursa ya kuidhamini klabu hiyo ya Yanga.
Licha ya usiri mkubwa kutawala kwenye kikao hicho, BINGWA limefanikiwa kunasa orodha ya baadhi ya kampuni ambazo zilijitokeza kwenye mkutano huo ambao ulioendeshwa na Kampuni ya Purple Cow Media chini ya Mkurugenzi wake, Akrati Bhargava, ukiwa na lengo la kuyapa fursa makampuni hayo na kubadilishana mawazo na kuangalia ni namna gani wanaweza kuidhamini klabu hiyo.
Gazeti hili liliwahi kuripoti kuwa lengo kubwa la mkutano huo lilikuwa ni kuwaeleza dhamira ya kuwapa fursa wafanyabiashara na kampuni hizo kuidhamini Yanga kupitia nembo yake hasa kwa upande wa jezi za timu hiyo ili klabu hiyo iweze kuwa na wadhamini wengi.
BINGWA wiki iliyopita lilimnukuu Bhargava akisema: “Tumechukua mfumo wa Manchester United, tunataka kuwa na wadhamini katika kila eneo, kuanzia jezi za mazoezini, kwenye mechi na mambo mengine na tunaona hili linawezekana kwani mkutano wetu huu umekua na manufaa sana.”
Katika orodha ambayo gazeti hili limeipata inaonyesha kuwa kampuni kadhaa kubwa zimevutiwa na wazo hilo na ndiyo maana zilijitokeza kwa wingi kushiriki mkutano huo ambao wadau wa soka wanaamini mafanikio yake yataibeba zaidi Yanga kimapato.
Baadhi ya kampuni ambazo zilikuwa na uwakilishi kwenye mkutano huo ni pamoja na kampuni ya AIM Group, Avic Coastland Development (T) LTD, R & R Associates, Strictly Communication, Kileki Enterprise na Mac Travel Agency.
Kampuni nyingine zilizokuwa na wawakilishi kwenye mkutano huo ni Aggrey and Clifford, G4S Secure Solution, Tanzania, PinPoint African Media, Advent Constructions Ltd, Makgroup of Companies Tanzania.
Kwa upande mwingine kampuni ya bia ya SBL Subsidiary of EABL/DIAGEO PLC, ilikuwa na mwakilishi sambamba huku hoteli ya kitalii ya Jangwani Sea Breez Resort nayo pia ikiwakilishwa kwenye mkutano huo wa kuchangamkia fursa za kuidhamini Yanga.
Mabenki nayo hayakuwa nyuma kwenye mkutano huo ambapo benki ya Posta, Eco Bank, Amana Bank Limited na Exim Bank Tanzania Ltd nazo pia zilikuwa na wawakilishi kwenye mkutano huo ambao ulikuwa na dhumuni la kuifanya Yanga kuwa ya kimataifa zaidi.
BINGWA ambalo siku ya mkutano huo lilipiga kambi kwenye hoteli hiyo, linafahamu kuwa mkutano ule ulikuwa na dhumuni la kuzieleza kampuni hizo namna ya kudhamini klabu hiyo kwenye sekta mbalimbali zikiwemo afya, benki na suala nzima la nembo kwenye jezi za klabu hiyo.
Yanga ipo kwenye mchakato wa kubadili mfumo na kuondokana na mfumo wa sasa wa kutegemea misaada ya wafadhili na viingilio vya mlangoni ambavyo vimeshuka kutokana na mechi za ligi kuu kuonyeshwa katika televisheni.


Post a Comment

 
Top