UNAIJUA SIMBA AU UNAISIKIA tu, huu ndio ujumbe ambao klabu ya Simba imeutuma kwa wanaoibeza kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting katika mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo, Simba walipata mabao yao kupitia kwa mastraika wake, Ibrahim Ajib na Laudit Mavugo, wakati lile la Ruvu Shooting likiwekwa kimiani na Ibrahim Mussa.
Mechi hiyo ilianza kwa kasi kwa timu zote kushambuliana kwa zamu, ambapo  dakika ya tatu beki wa Simba,  Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, alishindwa kumalizia pasi ya mwisho ya Mwinyi Kazimoto na shuti lake kutoka nje.
Ruvu Shooting walipata bao la kuongoza dakika ya nane ya mchezo huo kupitia kwa Mussa ambaye alimzidi ujanja beki wa Simba, Method Mwanjali, kabla ya kumhadaa kipa Vincent  Angban na kupiga shuti  lililokwenda moja kwa moja nyavuni.
Baada ya kufungwa bao hilo, Simba walicharuka na kupata bao la kusawazisha dakika tatu baadaye kupitia kwa Ajib aliyefunga akimalizia krosi kutoka winga ya kushoto iliyochongwa na Tshabalala.
Simba waliendelea kulisakama lango la Ruvu na katika dakika ya 15, Mavugo alishindwa kufunga baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Ajib akiwa kwenye eneo zuri, lakini shuti lake liliokolewa na kipa, Abdallah Abdallah.
Kombinesheni ya Ajib na Mavugo iliendelea kuitesa beki ya Ruvu na katika dakika ya 19, Ajib alimtengenezea nafasi nzuri Mavugo ambaye alishindwa kuitumia baada ya kupiga shuti ambalo lilipaa juu ya lango.
Katika dakika ya 26, Ruvu walifanikiwa kutengeneza nafasi ya kufunga, lakini Claide Wigenge alishindwa kumalizia kazi nzuri ya Abrahaman Musa baada ya shuti lake kuokolewa na Angban.
Katika mchezo huo utatu wa Said Ndemla, Jonas Mkude na Mwinyi Kazimoto, ulionekana kukamata eneo la kiungo, huku wakionana vizuri na kutengeneza mashambulizi ya mara kwa mara langoni kwa wapinzani wao.
Uamuzi wa kocha wa Simba, Joseph Omog kumwanzisha Ndemla kwenye pambano hilo, ulionekana wa busara kutokana na staa huyo kupiga mpira mkubwa sana katikati ya uwanja na katika dakika ya 36 krosi yake kwa Mavugo nusura izae bao lakini Mrundi huyo alikosa umakini.
Ruvu walifanya shambulizi zuri dakika ya 38, lakini Claude Wigenge alichelewa  kumalizia  krosi ya Shabani Kisiga baada ya mpira kutoka nje.
Dakika ya 44, Ajib alitoa pasi  kwa Kichuya, lakini alipiga shuti hafifu  na  kutoka nje ambapo  Mavugo alifunga bao la pili dakika ya 48 kutokana na pasi ya Ajib.
Kipa wa Ruvu, Abdallah alifanya kazi nzuri dakika ya 56 baada ya kuokoa shuti la Ndemla ambao lilionekana kwenda wavuni.
Simba waliendelea kufanya mashambulizi langoni mwa Ruvu na dakika ya 66, Mwinyi alipiga krosi iliyomkuta Blagnon, lakini alishindwa kufunga kwa kichwa baada ya kipa wa Ruvu kuokoa hatari hiyo.
Ajib alishindwa kufunga dakika ya 76 baada ya Blagnon kumtengea pasi, lakini shuti lake liligonga mwamba na kipa wa Ruvu anadaka.
Dakika ya 79, Jabir Aziz wa Ruvu alionyeshwa kadi nyekundu na Mwamuzi Ngole Mwangole, baada ya kumwangusha Mzamir Yassin kwenye eneo la hatari ambaye awali alikuwa na kadi ya njano.
Katika hatua nyingine, baadhi ya matajiri wa klabu ya Simba wanatarajia kuwakabidhi wachezaji wa klabu hiyo kiasi cha shilingi milioni 10 kama pongezi kwa ushindi huo muhimu.
Matajiri hao ambao wamejiwekea utaratibu wa kuchangishana na kukusanya kiasi cha milioni 10 ambacho hukitoa kwa wachezaji katika kila mechi ambayo watashinda, lakini kama wakifungwa au kutoa sare fedha hizo zinahifadhiwa.

Post a Comment

 
Top