KILICHOIUA YANGA HIKI HAPA
HALI ya Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara kwa kiasi kikubwa imechangia mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Yanga kushindwa kuonyesha kiwango chao cha siku zote na kujikuta ikibanwa mbavu ugenini na Ndanda FC.
Hayo yalisemwa jana na kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, mara baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Ndanda uliopigwa katika uwanja huo na timu hizo kwenda suluhu ya bila kufungana.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mchezo huo, Mwambusi alisema Uwanja wa Nangwanda Sijaona si rafiki (hauna ubora) na ndiyo maana wachezaji wake wameshindwa kucheza soka lao lililozoeleka siku zote.
“Kiukweli sehemu ya kuchezea ya uwanja huu si rafiki kwa mchezaji kuonyesha kiwango chake halisi, ndiyo maana leo vijana wetu wameshindwa kuonyesha viwango vyao vilivyozoeleka.
“Lakini tunashukuru tumepata hii pointi moja ugenini kwa sababu si mbaya sana na sasa akili zetu tunazielekeza kwenye mechi inayofuata dhidi ya Majimaji,” alisema Mwambusi.
Mchezo wa jana ulianza kwa kasi kila upande ukitafuta bao la ushindi, lakini hakuna ambayo ilifanikiwa kuona lango la mwenzake zaidi ya dakika 45 za kwanza kutawaliwa na faulo za mara kwa mara.
Katika dakika ya 25, straika wa Yanga, Mzambia Obrey Chirwa, alikosa bao la wazi baada ya kupokea pasi safi ya Donald Ngoma, lakini mpira aliopiga ulikuwa dhaifu na kuokolewa na mabeki wa Ndanda.
Kwa upande wa pili, Ndanda nao walijaribu kufanya mashambulizi ya kushtukiza langoni mwa Yanga, lakini beki Andrew Vincent ‘Dante’ alikuwa kwenye ubora wa hali ya juu na kuokoa hatari kutoka kwa wapinzani wao ikiwemo shuti la Omary Mponda lililokuwa linaelekea golini.
Salum Minely alipewa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi Ngoma huku Kigi Makasy akizawadiwa kadi pia baada ya kumcheza rafu mbaya Simon Msuva na kwa upande wa Yanga, Deus Kaseke naye alilimwa kadi ya njano.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi Yanga wakionekana kulisakama lango la Ndanda lakini umaridadi wa safu ya ulinzi ukatibua mipangilio yao yote.
Kipindi cha pili Yanga walifanya mabadiliko kwa kumtoa Kaseke na kumwingiza Juma Mahadhi ili kuimarisha safu ya kiungo, huku dakika ya 66 Ndanda wakimtoa Salum Minely na kuingia Nasoro Kapama.
Post a Comment