Beki wa kulia wa Simba, Hamad Juma akimtoka kiungo wa Ndanda FC, Salum Telela
KOCHA Mkuu wa Ndanda FC, Amimu Mawazo ametamba kuwa timu yake hiyo itaisambaratisha Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaozikutanisha timu hizo Jumatano hii katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
Majigambo hayo ya Mawazo yanatokana na kuwa na mchezaji wa zamani wa Yanga, Salum Telela ambaye alidai kuwa anaijua vilivyo timu hiyo, hivyo anaamini kabisa atakiongoza vilivyo kikosi chake hicho kuibuka na ushindi katika mchezo huo.
Msimu uliopita, Telela aliitumikia Yanga katika ligi hiyo lakini baadaye alifungashiwa virago baada ya kudaiwa kuwa kiwango chake kimeporomoka ndipo alipoamua kwenda kujiunga na Ndanda FC.
Mawazo alisema kuwa tayari ameshamkabidhi Telela majukumu ya kufanya katika mechi hiyo ambayo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
“Tunaendelea vizuri na maandalizi yetu kwa ajili ya mchezo huo, lakini ni matumaini yetu kuwa tutaibuka na ushindi katika mchezo huo ili tuweze kujiweka katika nafasi nzuri zaidi kwenye msimamo wa ligi.
“Matumaini hayo yanatokana na uwepo wa Telela katika kikosi changu ambaye anaijua vizuri Yanga na tayari nimeshampatia majukumu ya kufanya ili kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema Mawazo.

Kikosi cha Yanga kitaondoka leo Jumatatu jijini Dar es Salaam na kwenda Mtwara kwa ajili ya mchezo huo.

Post a Comment

 
Top