LICHA
ya uwezo wa kufunga na kutengeneza mabao mengi, kiungo mkongwe nchini, Haruna
Moshi ‘Boban’, alitemwa na Mbeya City mwishoni mwa usajili wa msimu huu, lakini
kocha amefunguka nje ndani sababu za kumuacha.
Boban
alikuwa mhimili mkuu ndani ya kikosi cha Mbeya City msimu uliopita akicheza
kama kiungo na wakati mwingine kama mshambuliaji wa pili, lakini hiyo
haikusaidia kupewa mkataba mwingine.
Kocha
Kinnah Phiri raia wa Malawi amelielezea Championi Jumatatu sababu kuu tatu
zilizomnyima Boban mkataba mwingine kwa kile alichosema ni jazba, umri na
falsafa ya kiufundi.
“Kweli
Boban alitusaidia lakini naye kama binadamu alikuwa na udhaifu wake. Sawa,
alikuwa na nidhamu lakini hakujua kuitumia. Ni mtu wa jazba aliyependa kulipiza
kwa hasira nyingi, jambo ambalo lilikuwa likileta sura tofauti. Pia pamoja na
kiwango kizuri, Boban alikuwa hajitumi kama wakongwe wenzake kama Redondo
(Ramadhan Chombo).
“Lakini
pia, tayari umri ulikuwa umekwenda na kutokana na falsafa yangu ya kupendelea
zaidi damu changa na wakongwe wachache sana kwenye kikosi changu, ndiyo maana
akawa mmoja wa wale walioachwa,” alisema Phiri.
Msimu
huu Phiri anasema amebakiza wakongwe wanne tu; Juma Kaseja, Redondo, Andrew
Chaima na Hassan Mwasapili.
Post a Comment