TIMU ya soka ya Simba inatarajiwa kucheza
mchezo wa kirafiki dhidi ya Polisi Dodoma, katika mpambano unaotarajiwa kufanyika leo kwenye Uwanja wa
Jamhuri mjini hapa.
Pambano hilo limeandaliwa maalumu ikiwa ni
sehemu ya kuiandaa Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting
utakaochezwa Jumatano ya wiki ijayo jijini Dar es Salaam.
Mashabiki wa mjini hapa hawajaiona Simba tangu
msimu wa 2011-2012 walipocheza mchezo wa mwisho wa ligi.
Wakati Simba watakua wakiutumia mchezo huo
kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara, wapinzani wao Polisi Dodoma watautumia
kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Daraja la Kwanza mchezo wa ufunguzi dhidi ya
Panone ya Kilimanjaro, Septemba 24 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, kocha
msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, alisema mchezo huo ni kwa ajili ya kuwapima
wachezaji wao.
Wachezaji wa kimataifa atakaowatumia katika
mchezo huo ni Vincent Angban na Fredrick Blagnon wote kutoka Ivory Coast,
Method Mwanjali kutoka Zimbabwe na Wakongo, Besala Janvier Bukungu na Mousa
Ndusha.
Mayanja alisema wachezaji waliopo na timu za
taifa ni Laudit Mavugo (Burundi) na Jjuuko Murshid (Uganda), wakati Shiza
Kichuya, Ibrahim Ajib, Mohamed Ibrahim, Mohammed Hussein ‘Tshabalala na Jonas
Mkude wapo kwenye kikosi cha Taifa Stars.
Alisema atautumia mchezo huo kuwaangalia
wachezaji wake wapya pamoja na kutengeneza kombinesheni ya uchezaji kutokana na
wachezaji wengi kuwa wapya.
“Natengeneza ‘combination’ ya timu, sasa
huwezi kuitengeneza sehemu nyingine zaidi ya michezo ya kirafiki kama hii,
niwaombe mashabiki waje waone burudani,” alisema Mayanja.
Kocha wa timu ya Polisi Dodoma, Paul
Domishian, kwa upande wake alisema mchezo huo una hadhi na unaendana na malengo
yao ya kucheza Ligi Kuu Bara hivyo watautumia kutengeneza timu yake.
Post a Comment