HIVI karibuni mshambuliaji wa Simba, Mrundi, Laudit Mavugo, alipata fursa ya kuangalia jinsi Mrundi mwenzake wa Yanga, Amissi Tambwe alivyokuwa akizifumania nyavu katika michuano ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita.
Mavugo alikuwa akiyaangalia mabao hayo kupitia Mtandao wa YouTube ambako mabao yote aliyofunga Tambwe msimu uliopita yanapatikana.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba zimedai kuwa Mavugo alipagawa baada ya kuyaona mabao hayo na kujikuta akimmwagia sifa mbele ya wachezaji wenzake waliokuwa wakiangalia naye video hiyo.
“Hivi karibuni tulikuwa tunaangalia video ya mabao ya Tambwe katika Mtandao wa YouTube ambapo kuna mabao yake yote 21 aliyofunga msimu uliopita.
MAVUGO
“Hata hivyo, Mavugo alipagawa baada ya kuona jinsi jamaa alivyokuwa akifunga, zaidi alivutiwa na mabao mawili aliyofunga katika mchezo dhidi ya Stand United mkoani Shinyanga kwa kutumia kichwa na mguu lakini pia bao alilofunga wakati walipocheza na Mbeya City huko jijini Mbeya.
“Kutokana na mabao hayo, Mavugo alisema kuwa jamaa anajua kufunga hata alipokuwa Burundi alikuwa akifanya vizuri lakini atapambana naye,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Alipoulizwa Mavugo  kuhusiana na suala hilo alisema: “Nimeyaona mabao hayo, ni mazuri, hivyo nampongeza kwa kazi hiyo.”
Kwa sasa wachezaji hao wapo kwao Burundi ambako wameenda kuitumikia timu yao ya taifa ambayo leo itakuwa ugenini kupambana na Niger.

Post a Comment

 
Top