KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Kinnah Phiri ametangaza kumuondoa kwenye program zake za msimu mzima kipa mkongwe, Juma Kaseja kufuatia kipa huyo kutoripoti kambini mpaka sasa tangu atoke Afrika Kusini alikokwenda na timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys.

Kaseja aliteuliwa kuwa kwenye benchi la U-17 iliyokuwa ikijiandaa na mchezo dhidi ya Afrika Kusini, wiki tatu zilizopita na tayari zimerudiana na Serengeti kufuzu kwa jumla ya mabao 3-1.


Phiri alisema mpaka hana taarifa rasmi kama mkuu wa benchi la ufundi aidha kutoka kwake wala viongozi wa timu hiyo, kitendo alichokiita ni utovu wa nidhamu na hatua inayofuata ni kumuondoa kwenye program ya msimu mzima.

Aliongeza kuwa Kaseja hajaonekana kikosini tangu kwenye maandalizi ya msimu (pre seasons) mpaka sasa wakiwa wamecheza mechi mbili za ligi kuu huku akitarajia kuikosa pia mechi dhidi ya Mbao FC itakayopigwa kesho Jumamosi mkoani Mwanza.

“Kama ni taarifa zake ninajua alikuwa na kikosi cha Serengeti Boys na tayari wamerudi muda mrefu lakini mwenyewe hajaripoti kambini. Sijui sababu na wala hajanipa taarifa wala viongozi wa juu.

“Siyo kwamba nina hofu na wachezaji nilionao, lakini kitendo hicho ni utovu wa nidhamu na siko tayari kuvumilia vitendo vya namna hii.

“Iwapo ataamua kurudi mwenyewe na kama hatokuwa na sababu za msingi, lazima atumikie adhabu, ikiwemo kuondolewa kwenye program za msimu wa ligi maana hajafanya program yoyote na ligi ndiyo inaendelea kuwa ngumu,” aling’aka kocha huyo wa zamani wa Free Staes ya Afrika Kusini.

Kabla ya kutua Mbeya City, Kaseja aliyewahi kutwaa Tuzo ya Kipa Bora wa Msimu mara mbili aliondoka Yanga ‘kimazabe’ baada ya kuweka mgomo wa kurejea kikosini akishinikiza kulipwa fedha zake za usajili huku pia ishu ya kupigwa benchi na makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deo Munish pia kilichangia.
CHAMPIONI

Post a Comment

 
Top