MSHAMBULIAJI wa zamani wa
Yanga na Azam FC, Mrundi, Didier Kavumbagu ameamua kumueleza ukweli
mshambuliaji wa Simba, Mrundi, Laudit Mavugo kuhusiana na kiwango alichonacho
na nini cha kufanya kama kweli anataka kufanikiwa katika Ligi Kuu Bara.
Kavumbagu ambaye amecheza
mechi kadhaa na Mavugo wakiwa wote timu ya taifa ameanza kwa kueleza kuwa kwa
tathmini yake mshambuliaji huyo anamwona ni wa kawaida tofauti na sifa
anazozisikia akipewa na watu wengine.
“Mavugo ni straika wa kawaida, siwezi kusema ni hatari sana kama anavyozungumziwa na wengine. Nayasema haya kwa kuwa ninamfahamu tangu tukiwa tunakutana timu ya taifa mpaka anakuja Tanzania.
“Anapaswa kuelewa kuwa
amekuja kwenye ligi ya Tanzania, haitaji mazoezi ya timu pekee na kipaji
alichonacho kama kweli anataka kufanikiwa akiwa hapa. Anahitaji kufanya mazoezi
ya ziada na awe na nidhamu ya hali ya juu, vinginevyo atasahaulika muda si
mrefu.
“Ishu ya kuonekana yeye ni
hatari, tayari watu wameshaamini hivyo kwamba yupo vizuri sana, sasa anahitaji
kulithibitisha hilo na hilo lipo mikononi mwake, anatakiwa apambane kuonyesha
kuwa mashabiki hawakukosea kuamini kuwa ni straika hatari.
“Sitaki kuzungumzia kuhusu
ushindani kati yake na Amissi Tambwe (wa Yanga), lakini kwenye timu ya taifa
mimi na Tambwe huwa tunaanza kikosi cha kwanza na yeye (Mavugo) anakuwa benchi,
sasa kwa hivyo inatosha kufahamu ushindani uliopo mbele yake kwa sababu huwa
sipendi kufananisha vitu,” alisema Kavumbagu.
Post a Comment