Mkwasa ataja kilichoiua Stars
BAADA ya kukumbana na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Nigeria katika mchezo wa kutafuta nafasi ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON), Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Charles Boniface Mkwasa, ameanika kilichowasibu.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkwasa alisema kuwa sababu zipo nyingi zilizopelekea wakakumbana na kipigo hicho kutoka kwa miamba hiyo ya Afrika Kaskazini.
Alisema kuwa kitendo cha kutopewa muda wa kufanya maandalizi ya kutosha ni sababu tosha ya kutofanya vizuri katika mcheo huo, ikizingatiwa kuwa walifanya maandalizi ya siku mbili.
“Maandalizi tuliyofanya ni ya muda mfupi mno, ikizingatiwa kuwa tunakutana na kikosi chenye wachezaji wenye majina na uzoefu kama Nigeria,” alisema.
Alisema kuwa kitendo walichokifanya Shirika la Ndege la Ethiopia, Ethiopian Airline cha kushindwa kuwatafutia sehemu ya kulala wachezaji wake na kuwalaza kwenye mabenchi kiliondoa ari katika kikosi chake.
“Wachezaji wangu hawakujisikia vizuri kwa kitendo kisichokuwa cha kiungwana, shirikisho linapaswa kuwahoji ilikuwaje hali hii ikajitokeza,” alisema.
Alisema kuwa kikosi chake kilikumbwa na matatizo mengi ndani na nje ya uwanja, kwani katika mchezo huo kikosi kilikwenda na jezi pea moja, kitu kilichowapa wakati mgumu pindi walipoingia uwanjani kumalizia kipindi cha pili, kwani walilazimika kuvaa jezi zilizolowa, jambo ambalo halipendezi.
Kwa upande wa suala la beki Kelvin Yondani, Mkwasa alisema kuwa hawezi kumpa adhabu mchezaji huyo, kwani kama hayupo tayari atampa nafasi mchezaji mwingine wa kuziba nafasi yake.
Post a Comment