HUKU habari za beki Mrundi kutoka Gor Mahia ya Kenya, Abdul Karim Nizigiyimana Makenzi kujiunga na kikosi cha Simba zikiwa bado mpya, tayari beki huyo ametangaza kazi muhimu atakayowafanyia Wanamsimbazi hao endapo watafikia muafaka.
Nizigiyimana, mwenye umri wa miaka 27, amewahakikishia Simba kwamba miongoni mwa mambo atakayofanya ni kuhakikisha anazuia madhara yatakayotokana na straika wa Yanga, Amis Tambwe, ambaye anadai anamfahamu vizuri.
Nizigiyimana na Tambwe kwa nyakati tofauti wameshacheza pamoja katika kikosi cha timu ya Taifa ya Burundi, hivyo beki huyo amedai anafahamu mbinu zake zote na pia anajua jinsi ya kumkabili ili asilete madhara.
Simba imeonyesha nia ya kumsajili beki huyo ili kuziba nafasi ya Hassan Ramadhani Kessy, aliyehamia Yanga, huku wakiachana na beki mwingine Mrundi, Emily Nimuboma.
Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, alikataa kuweka wazi kuhusu usajili wa beki huyo kwa kile alichodai timu yake kwa sasa inaangalia michuano ya ligi, lakini DIMBA Jumatano linafahamu kwamba tayari Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu, ameshafanya mazungumzo mara kadhaa na beki huyo kwa ajili ya kumshawishi ajiunge na Wekundu hao wa Msimbazi.
Habari ambazo DIMBA Jumatano linazo zinasema endapo klabu hiyo itafikia makubaliano na beki huyo, basi italazimika kuachana na beki mwingine, Javier Besala Bokungu, ambaye hadi sasa hajacheza mchezo hata mmoja wa ligi kutokana na kutokamilika kwa vibali vyake, licha ya Wekundu hao wa Msimbazi kumsainisha mkataba wa miezi sita.

Post a Comment

 
Top