Simba yote yahamia Taifa
SIMBA wanakereka sana na suluhu ya 0-0 waliyoipata mchezo wao uliopita dhidi ya Maafande wa JKT Ruvu na sasa wamejikusanya kisawasawa kuhakikisha wanamalizia hasira zao zote watakapowakabili Ruvu Shooting leo. Na uongozi wa klabu hiyo umewataka mashabiki wote kufika uwanjani kwa wingi ili kuishangilia timu yao iweze kuibuka na ushindi.
Wekundu hao wa Msimbazi watashuka kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Uhuru kumenyana na Maafande hao ikiwa ni mchezo wa raundi ya tatu ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, unaotarajiwa kuwa mgumu kutokana na kila timu kupania kupata matokeo mazuri.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Uwanja wa Uhuru umeanza kutumika kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom na zile za Ligi Daraja la Kwanza, ambapo mechi ya kwanza kuchezwa kwenye uwanja huo itakuwa ni ya leo kati ya Simba na Ruvu Shooting.
Simba ambao waliianza Ligi kwa kishindo kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ndanda FC, kwa sasa wanashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi hiyo wakiwa na pointi nne, huku Mbeya City wakiwa kileleni na pointi zao saba.
Katika mchezo huo, Simba itaitegemea zaidi safu yake ya ushambuliaji inayoundwa na Mrundi Laudit Mavugo, Ibrahim Ajib pamoja na Muivory Coast Frederick Blagnon, ambao wameandaliwa vilivyo kupachika mabao mengi iwezekanavyo.
Kocha Mkuu wa kikosi hicho aliwahi kuliambia gazeti hili kuwa amewaambia wachezaji wake kuhakikisha hawamalizi dakika 45 za kipindi cha kwanza bila kufunga bao lolote na hii ni katika kila mchezo watakaocheza.
“Ni vizuri sana timu inapopata mabao ya mapema, kwani inawapa wachezaji kujiamini, ndiyo maana nimewaambia kila mchezo wahakikishe kabla ya kwenda mapumziko wawe wameshafunga angalau bao 1-0, nadhani hilo linawezekana,” alisema.
Simba wataingia katika mchezo huo wakiwa na ari ya ushindi, hasa baada ya kutoka suluhu ya 0-0 mchezo wao uliopita wa Ligi dhidi ya JKT Ruvu, huku wakishinda mabao 2-0 mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Polisi Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mchezo huo dhidi ya Polisi Dodoma uliochezwa mkoani humo ulimpa fursa kocha mkuu wa kikosi hicho, Joseph Omog, kuwatumia wachezaji wake ambao wamekuwa wakisugua benchi na hii ni baada ya wale wa kikosi cha kwanza wengi wao kuwa katika timu zao za Taifa.
Wakati Simba wakijitapa kuibuka na ushindi huo, kwa upande wao Ruvu Shooting wamezisikia kelele hizo na kisha nao wakachimba mkwara mzito wakisema kuwa Wekundu hao wa Msimbazi hawataamini kitakachowatokea.
Msemaji wa kikosi hicho, Masau Bwire, alisema: “Waambieni hao Simba kelele zao tutazizima, kwani tunasikia kuwa wanachonga sana huko mjini, sisi tumejiandaa kikamilifu na hawataamini kitakachowatokea.”
Timu hizo zilipokutana mara ya mwisho msimu wa 2014/15 Simba walishinda michezo yote miwili, wakianza na ushindi wa bao 1-0 mchezo wa mzunguko wa kwanza na kushinda mabao 3-0 mzunguko wa pili ambapo msimu uliopita maafande hao walikuwa Ligi Daraja la kwanza.
Post a Comment