Mabilionea wapigana vikumbo Yanga
YANGA leo inaweza kujikuta ikifungua ukurasa mpya utakaoifanya kusahau kabisa ukata au kujiendesha kihasara kutokana na idadi kubwa ya wafanyabiashara mabilionea kutarajiwa kujitokeza kupigana vikumbo kuidhamini.
Mabilionea hao yakiwamo makampuni makubwa nchini, wanakutana leo kwenye Hoteli ya Double Tree, Dar es Salaam kuona ni vipi kila mmoja anaweza kuwabwaga wenzake katika suala zima la dau la kuidhamini klabu hiyo.
Yanga ipo katika mkakati wa kujiendesha kibiashara ili kuondokana na mfumo wa sasa ambao unaifanya klabu hiyo kutegemea mtu mmoja katika kujiendesha.
Huu ni mkakati ambao utaifanya Yanga kujiendesha kibiashara na kuondokana na mfumo wa sasa wa kutegemea misaada ya wafadhili na viingilio vya mlangoni ambavyo vimeshuka kutokana na mechi za Ligi Kuu kuonyeshwa katika televisheni.
Simba na Yanga zimejikuta zikilazimika kutaka kujiimarisha zaidi kiuchumi hivyo kuwa na uwezo wa kuvisuka vikosi vyao na kuwa tishio barani Afrika ikiwa ni matokeo ya mkakati kabambe wa Rais John Magufuli wa kuimarisha uchumi nchini.
Tangu Rais Magufuli alivyoingia madarakani Oktoba mwaka jana, amekuwa akihimiza kwa nguvu zote ukusanyaji wa kodi lakini pia kudhibiti mianya yote ya rushwa na kila aina ya wizi kama sehemu ya kuimarisha usimamizi wa mali na fedha za Serikali.
Kutokana na hali hiyo, wafanyabiashara wengi wamekuwa wakiumiza vichwa kuona ni vipi wanaweza kuzinadi bidhaa au huduma zao ili waweze kupata soko litakalowawezesha kuendelea na shughuli zao.
Baada ya mfanyabiashara, Mohamed Dewji ‘Mo’ kujitokeza kutaka kununua hisa za klabu ya Simba, kwa upande wa Yanga akajitokeza bilionea anayetaka kumiliki nembo ya klabu hiyo, makampuni na mashirika kadha wa kadha yameanza kuzigombania klabu hizo ili kuzidhamini ziweze kuzitumia kama ubao wa matangazo ya kunadi bidhaa zao.
Japo hakuna kiongozi yeyote wa Yanga aliyeweka wazi nini hasa kitajiri katika mkutano huo, lakini BINGWA katika nusanusa yake, limebaini kuwa kikubwa kitakuwa ni kujadili jinsi ya kuiwezesha klabu hiyo kujiendesha kibiashara zaidi hali ambayo ni wazi itawaingiza ‘vitani’ vibopa hao kila mmoja kutaka kuonyesha jeuri yake ya fedha.
Tayari imewekwa wazi kuwa moja ya makampuni yaliyo tayari kuingiza mamilioni yao Yanga ni Quality Group, Benki ya NBC na kampuni ya saruji ya Dangote ambayo inamilikiwa na bilionea namba moja barani Afrika, Aliko Dangote na mengine mengi, wakati pia wakiwamo wafanyabiashara mmoja mmoja ambao hata hivyo bado ni siri kubwa ndani ya klabu hiyo hadi leo usiku.
Hafla hiyo inatarajiwa kuanza saa 10 jioni hadi saa 1 moja usiku katika Hotel ya Double Tree.
Post a Comment