SIMBA ipo katika nafasi ya kuweka historia ya aina yake kwa kuwa timu ya kwanza Tanzania kutoa wachezaji watakaoshiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika 2017, hali inayoweza kuifanya kuwa kivutio kwa mawakala kutoka kila pembe ya dunia.

Fursa hiyo imekuja kupitia wachezaji wa timu hiyo waliopo katika kikosi cha Uganda ambacho wikiendi hii kitacheza na Comoro mchezo ambao iwapo itashinda, itakuwa imefuzu fainali hizo za Afrika.

Wachezaji ambao wanaelekea kuipa heshima hiyo Simba ni beki wa Wekundu wa Msimbazi hao, Juuko Murushid na nyota wa zamani wa klabu hiyo ambaye kwa sasa anakipiga nchini Denmark, Emmanuel Okwi.
Tayari Uganda imefikisha pointi 10 katika kundi D ambapo iwapo itaichapa Comoro wikiendi hii, itakuwa imefuzu fainali hizo za Afrika, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu nchi hiyo ilipofanya hivyo mwaka 1978.
Kwa upande mwingine, kitendo cha Murushid na Okwi kushiriki fainali hizo za Afcon 2017, kitawafanya mawakala wa soka kila pembe ya dunia kuitupia macho klabu hiyo ya Tanzania kuona kama wanaweza kupata wachezaji wengine wenye vipaji ili kuwauza Ulaya na kwingineko.

Uzoefu unaonyesha kuwa kila michuano hiyo ya Afrika inapofanyika, mawakala huitumia kuvuna vipaji hivyo pia inaweza kuwa fursa ya kipekee kwa Murushid na Okwi kujinadi zaidi iwapo watang’ara.

Hata hivyo, Uganda italazimika kutumia mbinu za ziada kuhakikisha wanashinda mchezo huo ambao wapo kundi moja na Burkina Faso, Botswana na Comoro.
Lakini iwapo itakubali kichapo itaipa nafasi Burkina Faso kusonga mbele kwa kuwa nao wana pointi 10 kama Uganda kwenye michuano hiyo.

Mbali na Uganda na Burkina Faso, timu nyingine zilizopo kwenye kundi hilo ni Botswana wenye pointi 6 na Comoro wanaoburuza mkia kwa pointi 3.

Post a Comment

 
Top