KOCHA wa Yanga, Hans van Der Pluijm, amempa ugumu
aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Free States ya Afrika Kusini, Mrisho Ngassa
kurejea kuichezea timu hiyo.
Hiyo, ni siku moja tangu taarifa za kiungo huyo kusitisha
mkataba wake wa kuichezea Free States kwa makubaliano huku tetesi zikienea kuwa
nyota huyo atarejea kucheza Yanga kwenye usajili wa dirisha dogo la Ligi Kuu
Bara msimu huu.
Ngassa, alisitisha mkataba wa kuendelea kukipiga Sauz
kwa kile alichodai kuwa timu hiyo haina malengo ya kutwaa ubingwa zaidi
kushiriki kwenye ligi kuu.
Pluijm alisema kwenye kikosi chake hahitaji kiungo
mshambuliaji kwani tayari anao wanne, tena vijana wenye uwezo mkubwa wa
kuendana na kasi yake.
Pluijm aliwataja viungo hao washambuliaji kuwa ni
Mzambia, Obrey Chirwa, Juma Mahadhi, Simon Msuva na Deus Kaseke ambao anaamini bado
wana uwezo mkubwa wa kuichezea timu hiyo kwa muda mrefu kutokana na umri wao.
Aliongeza kuwa, haoni sababu ya kujaza viungo wengi
washambuliaji kwenye kikosi chake kutokana na kutokuwa na tatizo katika nafasi
hiyo.
"Nimepata taarifa za Ngassa kusitisha mkataba wake
wa kuichezea Free States, labda nikwambie tu, ni ngumu kwangu kusajili kiungo
mshambuliaji katika kikosi changu kwa hivi sasa, kwani tayari ninao wanne ambao
ni vijana wenye uwezo mkubwa wa kucheza.
"Wachezaji wanaocheza nafasi hiyo (ya Ngassa) ni
Chirwa, Mahadhi, Kaseke na Msuva, wote ni wazuri. Tofauti na kasi yao ya
kushambulia, pia wana uwezo wa kufunga mabao, ni aina ya uchezaji aliyonayo
Ngassa," alisema Pluijm.
Post a Comment