UMATI wa mashabiki wa Yanga mkoani hapa, umemfanya kocha mkuu wa timu hiyo, Hans van der Pluijm, kushindwa kufanya mazoezi juzi kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Ndanda.
Pluijm alikataa kufanya mazoezi hayo, baada ya kuwataka mashabiki hao kuondoka uwanjani ili wapinzani wao wasipate nafasi ya kujua mbinu zake kabla ya mechi hiyo kuchezwa jana kwenye uwanja huo.
Yanga waliwasili mkoani hapa Jumatatu wiki hii wakilakiwa kwa mbwembwe za aina mbalimbali zikiwemo pikipiki na mashabiki wao huku kukiwa na ulinzi mkali.
Mashabiki hao walikuwa na shauku ya kuwaona baadhi ya wachezaji wao waliosajiliwa msimu huu, Juma Mahadhi, Ben Kalolanya, Obrey Chirwa, Andrew Vicent na Hassan Ramadhan ‘Kessy’.
Yanga ilikuwa ni mechi yao ya pili ya Ligi Kuu Bara kucheza baada ya kutolewa katika makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika walioshika mkia kutokana na pointi moja.
Timu hiyo iliyokuwa kwenye Kundi A pamoja na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Medeama ya Ghana na Mo Bejaia, ilianza ligi hiyo kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya African Lyon katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Post a Comment
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.