MIPANGO ya Yanga imetibuka, kwani haitaweza kumtumia beki wake kisiki, Vincent Bossou, ambaye ameng’ang’aniwa nchini kwao, Togo.
Yanga kwa muda mrefu imekuwa ikimtumia Bossou ambaye ni nahodha 
msaidizi kama beki kisiki, lakini mipango hiyo inaonekana kugonga mwamba
 wiki hii.
Juzi Bossou alikuwa na kikao kizito na uongozi wa Taifa lake 
kilichopelekea kuchelewa kurejea nchini kujiunga na kikosi cha timu ya 
Yanga ambacho kimeelekea mkoani Mtwara.
Yanga imeondoka jana asubuhi kuelekea mkoani humo kwa ajili ya mechi 
dhidi ya Ndanda FC, mchezo unaochezwa leo katika Uwanja wa Nangwanda 
Sijaona.
Bossou aling’ara kwenye kikosi chake mwishoni mwa wiki baada ya 
kufunga bao moja katika ushindi wa mabao 5-0 walioupata dhidi ya 
Djibouti kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 
mwakani nchini Gabon.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Kegue, mjini Lome, mabao ya 
The Sparrow Hawks yalifungwa na beki wa Yanga ya Tanzania, Vincent 
Bossou, Mathieu Dossevi, Fo-Doh Laba na Komlan Agbegniadan mawili na 
Togo inamaliza nafasi ya pili kwenye Kundi A hivyo kufuzu Afcon ya 
kwanza tangu mwaka 2013, baada ya Tunisia iliyoifunga Liberia 4-1 na 
kumaliza kileleni.
Akizungumza na DIMBA Jumatano jana kwa simu akiwa nchini Togo, Bossou
 alisema amefurahi kuisaidia timu yake ya taifa kuweza kufuzu kwa 
fainali hizo za Afcon, lakini hajui atarejea lini hapa nchini kujiunga 
na Yanga.
“Nafurahi kuona timu yangu imeingia moja kwa moja katika michuano 
hiyo, ni jambo la kujivunia, hata hivyo, sidhani kama nitawahi mechi za 
wiki hii kwa vile bado tuna vikao na viongozi wangu,” alisema.
Hii inakuwa mara ya kwanza kwa Togo kupata nafasi ya kushiriki Afcon 
tangu mwaka 2013 ilipofanikiwa kufika hatua ya robo fainali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
 


Post a Comment