MKURUGENZI wa Kituo cha Mkubwa na Wanawe na Diwani wa Kata ya Mbagala Kilungule (CCM), Said Fella ‘Mkubwa Fella’ amekata mzizi wa fitina kwa kuzionyesha nyumba nne mpya za wasanii wake wanaounda Kundi la Yamoto Band.
Nyumba hizo zipo Mbande Kisewe nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Wasanii wanaounda kundi hilo ni Dogo Aslay, Maromboso, Enock Bella na Beka Fleva ambao hawakuwepo eneo la tukio kutona na kuwa na majukumu nje ya nchi.
Fella alisema nyumba hizo zimekamilika kwa kiasi kikubwa kilichobaki ni umaliziaji wa kawaida wa ndani tu na pindi zitakapokamilika watazizindua rasmi na kuwakabidhi Yamoto, ambapo siku hiyo amedai atamualika aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Jakaya Kikwete kwa ajili ya kuzizindua.
Spotiripota ambayo lilikuwepo eneo la tukio lilishuhudia nyumba hizo mpya za kisasa zilizogharimu mamilioni ya fedha, zikiwa katika hatua za mwisho za ujenzi wake huku kila nyumba ikiwa na vyumba viwili vya kulala na ‘master’ moja, chumba cha chakula, jiko na stoo.
Fella alisema kuwa hiyo siyo mara ya kwanza kwake kuwajengea nyumba wasanii anao wasimamia kwani awali aliwajengea Juma Kasim ‘Juma Nature’, Said Juma ‘Chege’ na Aman Temba ‘Mh.Temba’ huku wengine wakimbulia kupata viwanja.
“Siku nyingi nilianza kutengeneza kituo changu cha Mkubwa na Wanawe nikiwa na mtu anaitwa Shoga Yake Mama akafuatia Dullah Yeyo mpaka nikampata Aslay kabla ya mwaka 2013 nilipoianzisha Yamoto Band baada ya kuwapata vijana wanne.
“Watu wengi wamenisaidia wakati ule ambao akina Chief Kiumbe, Ruge Mutahaba bila ya kumsahau rais wetu mstaafu Jakaya Kikwete
“Nilikuwa ninapata meseji nyingi za watu wakiuliza nimewafanyia nini Yamoto hivyo nimeamua kuwaita ili mjionee wenyewe nyumba hizi za vijana hawa kwa sababu maswali yamekuwa mengi sana,” alisema Fella.

Post a Comment

 
Top