HATIMAYE mshambuliaji mpya wa Yanga, Mzambia, Obrey
Chirwa, jana alitoa ‘gundu’ baada ya kufunga bao lake la kwanza tangu atue
kuichezea timu hiyo kwenye ushindi wa mabao 2-0.
Chirwa alifunga bao hilo wakati Yanga ilipocheza na timu
yao ya vijana chini ya miaka 20 yaani U20 inayofundishwa na beki na nahodha wa
zamani wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa.
Mzambia huyo, aliyetua kuichezea Yanga kwa dau la Sh milioni
200, amecheza mechi za Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe, Medeama
na MO Bejaia na nyingine ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar bila kufunga bao
lolote.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Viwanja vya
Gymkhana, Dar, mshambuliaji huyo, alifunga bao hilo katika dakika ya 17
akiunganisha krosi nzuri ya Thabani Kamusoko.
Chirwa amefunga bao hilo, akiwa ametoka kwenye majeraha
ya goti aliyoyapata kwenye mechi dhidi ya MO Bejaia na amerejea uwanjani juzi
Jumatatu.
Katika mechi hiyo, licha ya timu ya vijana kujitutumua
kutaka kusawazisha bao hilo, Mzimbabwe Donald Ngoma aliifungia Yanga bao la
pili kwa kumchambua kipa akipokea pasi ya Anthony Matheo.
Kikosi cha Yanga kiliundwa na Beno Kakolanya, Hassan
Kessy, Oscar Joshua, Juma Makapu, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kamusoko, Matheo,
Malimi Busungu, Chirwa, Ngoma na Yusuph Mhilu.
Post a Comment