BAADHI ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, juzi Jumatatu walivamia kambi ya timu hiyo na kushuhudia mchezo wa kirafiki kati ya Simba dhidi ya Burkinafaso inayoshirki Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara, huku Chuji na KMC wakiwavaa leo.
Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Highland mkoani hapa, ulimalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 5-0, ambapo mabosi hao wakiongozwa na katibu mkuu wa klabu hiyo, Patrick Kahemele, waliushuhudia mwanzo hadi mwisho.
Championi ambalo nalo lilikuwepo uwanjani hapo, baada ya mchezo huo, liliwashuhudia Kahemele, Musleh Al Rawah na Frisch Collins wakizungumza na Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog raia wa Cameroon.

 Hakuna aliyeweza kusikia wanazungumza nini kwani walikuwa wakiongea kwa siri kubwa, lakini mazungumzo yao yalichukua takribani dakika 30 mpaka kumalizika ambapo walionekana kujadili jambo huku wakicheka mara kwa mara.
Hata hivyo, hakuna kiongozi aliyekubali kuzungumzia kikao hicho kifupi.
Mbali ya kuwepo kwa viongozi hao waliokuwa wakizungumza na kocha, lakini pia mjumbe mwingine, Said Tully naye alikuwepo uwanjani hapo, lakini hakuwa sehemu ya mazungumzo na kocha.
Simba ambayo imepiga kambi mkoani hapa kwa takribani wiki ya tatu sasa, inatarajiwa kumaliza kambi yake leo Jumatano kwa kucheza mechi ya mwisho ya kirafiki dhidi ya KMC kutoka jijini Dar inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, kabla ya kesho Alhamisi kurudi Dar tayari kwa tamasha lao la Simba Day litakalofanyika Jumatatu ijayo.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa mashabiki wa soka hapa nchini kumshuhudia kiungo mahiri, Athumani Idd Chuji akiwa anaitumikia KMC lakini pia akicheza mchezo dhidi ya timu yake ya zamani Simba.

Post a Comment

 
Top