BENCHI la ufundi la Simba limeonekana kukuna vichwa kutafuta straika ambaye atakuwa pacha wa mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo, hasa baada ya kuonekana kutokuwepo kwa uelewano baina ya mshambuliaji huyo na washambuliaji wengine uwanjani.
Kocha wa Simba, Joseph Omog na Msaidizi wake, Jackson Mayanja, wameonekana kuwa katika wakati mgumu wa kumpata pacha wa Mavugo kutokana na kiwango cha washambuliaji wengine wa timu hiyo, Fredrick Blagnon na Ibrahim Ajib kuwachanganya makocha.
“Lazima tuchunguze na kuona nani hasa anaweza kucheza kwa ufanisi na Mavugo, tunafahamu kwamba wote ni wazuri, lakini nadhani kuna tatizo la kiufundi zaidi ambalo linapaswa kufanyiwa kazi na sisi makocha,” alisema Omog.
Kocha huyo raia wa Cameroon alisema kuwa Mavugo ana staili yake ya uchezaji ambayo ni vyema akapatiwa mtu sahihi wa kumsaidia, mtu ambaye atakuwa na kazi moja ya kuhakikisha mipira inafika kwa Mavugo kwa wakati sahihi.
“Ajib na Blagnon  ni wazuri sana, lakini kuna jambo linakosekana kati yao, hasa wanapocheza na Mavugo, lazima tuone nini kinakosekana kwa nani ili tupate mtu sahihi wa kucheza na Mavugo kama ilivyo kwa timu nyingine,” alisema.
Katika mchezo wa kwanza waliocheza Simba dhidi ya Ndanda FC, Blagnon, ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Ajib, alionekana kucheza vizuri, ingawa hakuweza kumchezesha vizuri Mavugo kama ilivyokuwa kwa Ajib, ambaye alicheza kipindi cha kwanza.
Katika mchezo wa juzi dhidi ya JKT Ruvu, Blagnon alianza pamoja na Mavugo, lakini mshambuliaji huyo raia wa Ivory Coast alionekana kushindwa kwenda na kasi ya mchezo hadi pale alipoingia Ajib na kuichangamsha safu ya ushambuliaji.
Kuingia kwa Ajib na Mwinyi Kazimoto kuliifanya Simba kutembea na kucheza soka safi baada ya mabadiliko, hali ambayo imepelekea benchi la ufundi la timu hiyo kuwa katika sintofahamu kati ya Ajib na Blagnon nani awe anaanza na nani awe anaingia.
Mayanja aliwahi kuliambia BINGWA kuwa wapo katika mkakati kabambe wa kumtafutia Mavugo pacha wake kutokana na aina yake ya soka analolicheza uwanjani.
“Bado Mavugo hajapata pacha wake halisi, ndiyo maana kila leo tunafanya mabadiliko katika kikosi, lakini muda si mrefu tutalitibu tatizo hili,” alisema Mayanja.


Post a Comment

 
Top