KUFUATIA makocha wa klabu za Simba
na Yanga kutoa maoni kuwa nyasi za Uwanja wa Uhuru kwamba ni hatari kwa
wachezaji kutokana na ugumu wa nyasi hizo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
limesema kuwa suala la timu hizo kuutumia uwanja huo katika mechi za Ligi Kuu
Bara, haliwezi kukwepeka kwa kuwa ulishafanyiwa ukarabati wa kutosha ukigharimu
mamilioni ya fedha.
Kocha wa Yanga, Hans van Der
Pluijm na Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, kila mmoja kwa wakati wake
alidai kuwa sehemu ya kuchezea ya uwanja huo bado tatizo kubwa ambalo linaweza
kusababisha wachezaji kupata majeraha.
Ofisa Habari wa TFF, Alfred
Lucas, alipoulizwa juu ya madai hayo alisema: “Kiukweli suala la kuutumia
uwanja huo haliwezi kukwepeka kwa timu yoyote ambayo itaanza kutoa visingizio.
“Umeshakamilika na upo tayari
kutumika katika michezo ya ligi kuu na lazima ifahamike wazi kwamba hao wanaosema
hivyo hakuna ambaye tayari ameshaumia.
“Lakini hilo tayari
lilishasemwa na Bodi ya Ligi mapema kabisa hata kabla serikali haijakabidhi,
sasa haliwezi kubadilika, hivi jamani watu hawaoni Uingereza kwamba ule Uwanja
wa Wembley unatumika katika mechi kubwa za heshima na ndiyo uwanja wa taifa! Tunataka
utumike hivyo katika mechi kubwa pekee, tena zile za kimataifa ila zilizobakia
utatumika huohuo,” alisema Lucas.
Post a Comment