NA SELEMAN SHINENI, BINGWA
YANGA ndivyo kama milivyosikia safari yao ya kuusaka ufalme wa Kombe la Shirikisho Afrika ilihitimishwa rasmi juzi kwa kile kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Licha ya kulipokea Kundi A kwa furaha kubwa, lakini safari yao ya kuliteka soka la bara la Afrika ilihitimishwa kwa wao kuburuza mkia wa kundi ambalo waliamini lilikuwa rahisi kwao kutokana na kutokuwa na timu nyingi za Kiarabu.

Wakiwa pamoja na timu za Mo Bejaia ya Algeria na Medeama ya Ghana, Yanga walijiaminisha kuwa watatinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho wakiwa sambamba na TP Mazembe.

Lakini, siku zote Waswahili wanasema ‘mipango si matumizi’ kwani katika mechi sita za Kundi A, Yanga walifanikiwa kuondoka na pointi nne tu, hii ni kutokana na kushinda mechi moja, kutoka sare moja na kufungwa nyingine nne.

Wakati Yanga wakiambulia pointi nne tu, Medeama SC ambayo wengi waliidharau ndiyo imemaliza katika nafasi ya pili ya Kundi A ikiwa na pointi nane na kusonga mbele sambamba na TP Mazembe walioongoza baada ya kuwa na pointi 13.

Medeama ilimaliza pointi sawa na Bejaia ambayo ilishika nafasi ya tatu, lakini ilibebwa na idadi kubwa ya mabao ya kufunga iliyokuwa nayo na kuwaacha Yanga wakiburuza mkia wakiwa na pointi zao nne tu.

Baada ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kuisha na Yanga kuyaaga rasmi mashindano hayo, BINGWA linakuleta makosa ambayo miamba hiyo ya Jangwani iliyafanya na kujikuta ikishindwa kufika nusu fainali ya mashindano hayo.

Mechi za nyumbani

Siri kubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika hasa hatua ya makundi ni kujua kuzicheza mechi zako za nyumbani, kwa sababu kati ya mechi sita za hatua hii tatu unacheza katika uwanja wako wa nyumbani hivyo kama ukishinda zote unakuwa na uhakika wa pointi tisa ambazo zinatosha kabisa kukuvusha kwenye kundi lako.

Lakini kwa Yanga hali haikuwa hivyo na ilishindwa kucheza mechi zake za Uwanja wa Taifa na kati ya pointi tisa ambazo ilitakiwa kuzivuna nyumbani iliambulia pointi nne na kupoteza nyingine tano (hii ni baada ya kushinda mechi moja, kutoka sare moja na kufungwa moja).

Wakati Yanga wakipata pointi nne nyumbani wapinzani wao, TP Mazembe kati ya pointi 13 walizovuna kwenye Kundi A, tisa wamepata nyumbani kutokana na kushinda mechi zao zote za Lubumbashi, Medeama wao kati ya pointi nane walizopata saba wamevuna nyumbani baada ya kushinda mechi mbili na kutoka sare moja katika mechi zao tatu walizocheza mjini Takoradi.

Mo Bejaia pia kwenye pointi nane walizovuna saba wamevuna nyumbani kwao na kupoteza pointi mbili tu katika ardhi ya mji wa Bejaia, huu ni ushahidi tosha kuwa wapinzani wa Yanga walijizatiti kupata matokeo mazuri nyumbani wakati vijana wa Hans van der Pluijm, wakishindwa kabisa kuutumia Uwanja wa Taifa.

Kupoteza nafasi

Kama umefuatilia mechi za Yanga katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho utakuwa umegundua kuwa vijana hawa wa Pluijm, walikuwa na tatizo la kushindwa kutumia nafasi walizozitengeneza kwenye mechi zao zote.

Karibu katika mechi zote za Yanga washumbuliaji wake walipata nafasi nyingi za kucheka na nyavu lakini walishindwa kuzitumia na mwisho wa siku timu ilipoteza mechi au kuambulia sare kitu ambacho kimekuja kuwaponza kwenye matokeo ya mwisho ya Kundi A na kuishia kuburuza mkia.

Kudharau kundi

Baada ya kuzikwepa timu za Uarabuni zilizokuwa na majina makubwa, Yanga wakadharau kundi lao la A wakiamini kuwa timu ambayo ilikuwa na uwezo wa kuwapa shida ilikuwa ni TP Mazembe pekee.

Dharau hii kwa kiasi kikubwa ilisababishwa na historia za kawaida za timu za Medeama na Mo Bejaia, hivyo timu kuna wakati ilijiandaa ikiwa na matokeo yake kichwani kitu ambacho kilikuja kuwatokea puani na kujikuta wakiteswa na miamba hiyo ya Ghana na Algeria kwa vipindi tofauti na kuishia kubeba wengine kwenye kundi lao.

Safu ya ulinzi

Licha ya kutajwa kama timu yenye safu bora ya ulinzi kwenye soka la Tanzania kwa sasa, Yanga imetupwa nje ya michuano hii ya Afrika kutokana na eneo hilo muhimu katika timu kufanya makosa ya aina ile ile mara kwa mara na kuiponza timu.

Yanga ambayo ndiyo imefungwa mabao mengi zaidi kwenye Kundi A ikiruhusu mabao tisa kwenye mechi sita, katika mechi zake nyingi ilikuwa ikiruhusu mabao ya aina ile ile ambayo mara kadhaa yalitokana na mipira iliyokufa, kitu ambacho kiliishia kuifanya timu ipoteze hata michezo ambayo ingeweza kupata sare na kuvuna pointi japo moja au kushinda kabisa.

Nidhamu

Kama kuna kitu kocha wa Yanga anatakiwa kukifanyia kazi wakati timu yake itakapoiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Afrika msimu ujao ni nidhamu.

Karibu katika kila mechi ya Yanga kwenye michuano ya Afrika msimu huu ilimkosa mchezaji wake muhimu mmoja au wawili kutokana na adhabu ya kadi mbili za njano au nyekundu.

Kitendo hiki kiliiumiza timu kwa sababu kila siku kocha alilazimika kutafuta mtu wa kuziba nafasi ambayo ilibaki wazi kutokana na kumkosa mchezaji wake muhimu na wakati mwingine mapengo hayo hayakuzibika ipasavyo na timu ikachezea kichapo.

Mechi za ugenini

Katika Kundi A lote ni Yanga pekee ambayo ilishindwa kuvuna japo pointi moja ugenini, wakati TP Mazembe kavuna nne, Medeama SC moja na Mo Bejaia moja kitu ambacho angalau kinathibitisha kuwa wapinzani wa miamba hiyo ya Jangwani walikuwa na mipango ya ugenini pia.

Siku zote kwenye mechi za makundi mbali na kushinda mechi za nyumbani timu inatakiwa kujipanga angalau kuambulia sare au hata ushindi mwembamba ugenini ili kujiweka vizuri kusonga mbele, pili msimu wa kundi ukiwekwa baada ya mechi za mwisho, lakini Yanga hawakuwa na hilo ndiyo maana pointi zake nne zote wamepata nyumbani tu.

Post a Comment

 
Top