BAO la winga wa Yanga, Juma Mahadhi, alilofunga katika mchezo wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya African Lyon mwishoni mwa wiki iliyopita, limewavutia matajiri wa klabu hiyo ambao wamefikia hatua ya ‘kulinunua’ kwa kumpa zawadi nyota huyo.
Mahadhi alifunga bao zuri katika mchezo huo baada ya kuchukua nafasi ya Simon Msuva, ambapo aliingia na hatimaye kuipatia bao la tatu timu yake hiyo ambayo iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Baada ya mechi hiyo winga huyo alifuatwa na mmoja wa wanachama matajiri wa klabu hiyo ambaye alitoka naye nje ya vyumba vya kubadilishia nguo na baada ya muda alirejea chumbani kwa ajili ya kusikiliza mawaidha ya kocha wao, Hans van Pluijm.
Baada ya kumalizika kwa mawaidha hayo, mchezaji huyo alichukuliwa na mmoja wa matajiri 17 wa Yanga ambaye ni mmoja wa wajumbe wa kamati ya mashindano iliyoteuliwa hivi karibuni, Mustapha Ulungo.
Mahadhi ni mchezaji pekee aliyechukuliwa na matajiri hao kutokana na jinsi walivyolikubali bao alilofunga mchezaji huyo kutokana na kutumia vyema umahiri wake akiwa mita 40.
Winga huyo alikuwepo katika eneo hilo la mita 40 ambapo alipiga shuti na kutikisa nyavu za African Lyon huku akimuacha kipa wa timu hiyo akijiuliza kutokana na umahiri wa bao hilo.
Post a Comment