MSHAMBULIAJI wa Simba, Mrundi, Laudit Mavugo, hivi karibuni
alionekana kama amelijaribu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kuvaa
jezi zenye namba mbili tofauti kwenye Ligi Kuu Bara.
Katika mchezo dhidi ya JKT Ruvu uliofanyika Jumamosi
iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Mavugo alivunja kanuni
ya shirikisho hilo baada ya kuvaa jezi namba 11 ambayo ilikuwa inavaliwa na
Mussa Mgos ambaye amestaafu soka.
Hii ilikuwa namba tofauti na ile ambayo aliivaa kwenye
mchezo dhidi ya Ndanda ambapo alivaa namba 9 ambayo ilisajiliwa kihalali kuwa
ni namba yake.
Kutokana na hali hiyo, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi
Tanzania (TPLB), Boniface Wambura, aliliambia Championi Jumatano kuwa, kitendo
hicho cha Mavugo kuvaa jezi zenye namba mbili tofauti katika mechi mbili
tofauti za ligi hiyo ni kosa kubwa, hivyo wanamchunguza na anaweza kuchukuliwa
hatua.
“Mchezaji mmoja kutumia namba mbili tofauti katika ligi ni
kosa kikanuni, hivyo kama Mavugo amefanya hivyo, basi atakuwa amevunja kanuni
hiyo.
“Hata hivyo, kwa sasa siwezi kulizungumzia sana suala hilo
kwa sababu bado halijanifikia mezani kwangu,” alisema Wambura kwa ufupi huku
pia akisita kuweka wazi adhabu ambayo Mavugo anaweza kukumbana nayo baada ya
kutenda kosa hilo.
Alipoulizwa Mavugo kuhusiana na suala hilo alisema: “
Binafsi sikujua kama ni kosa lakini ninachoweza kusema ni kwamba niliamua
kuitumia jezi namba 11 na kuachana na namba 9 kwa sababu nilikuwa nikiipenda.
“Lakini pia imeachwa na mtu ambaye mashabiki wengi wa Simba
walikuwa wakimpenda sana, hivyo na mimi kwa kuvaa jezi hiyo naamini nitawafanya
mashabiki wa timu yangu kuwa karibu na mimi zaidi.”
Post a Comment