SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema
endapo Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji ataendelea na msimamo wake wa kutaka
wanachama watatu wa klabu hiyo kufutwa uanachama wao, basi anaweza kufungiwa si
chini ya miaka 10.
Juni 6, mwaka huu, Klabu ya Yanga ilifanya
mkutano wa dharura ambapo Manji aliwafuta uanachama wanachama watatu wa klabu
hiyo ambao ni Ayoub Nyenzi, Salum Mkemi na Hashimu Abdallah, kutokana na sababu
zilizoelezwa kutaka kuihujumu Yanga.
Baada ya wanachama hao kufutwa uanachama,
wakaamua kupeleka malalamiko yao TFF wakidai mwenyekiti wao alikiuka katiba ya
klabu hiyo.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya TFF,
zinasema kuwa wanachama hao ambao pia ni Wajumbe wa Kamati ya Utendaji Yanga,
watarudishiwa uanachama wao na kuendelea na majukumu yao kama kawaida.
“Kila kitu kipo wazi, Nyenzi na wenzake
watarudishiwa uanachama wao na kurudi kwenye vituo vyao vya kazi kama kawaida
na endapo Manji atashikilia msimamo wake wa awali, basi atafikishwa katika
Kamati ya Maadili ya TFF na adhabu yake ni kifungo si chini ya miaka 10,”
kilisema chanzo hicho.
Wakati huohuo, Ofisa Habari wa TFF, Alfred
Lucas, amesema: “Kamati ya Maadili ya TFF inatarajiwa kukaa Jumapili hii
kuijadili ile barua iliyowasilishwa na wanachama wa Yanga waliofutwa uanachama.”
Chanzo: Championi
Post a Comment