LIGI Kuu ya England ‘Premier League’
inaendelea wikiendi hii ambapo vigogo wote watakuwa uwanjani kutafuta ushindi
huku gumzo ikiwa ni mchezo wa Tottenham dhidi ya Liverpool.
Mchezo huo ambao unatarajiwa kuchezwa
leo Jumamosi kwenye Uwanja wa White Hart Lane, utakuwa wa kwanza kabisa kabla
ya mechi nyingine kuchezwa jioni, huku ikikumbukwa kuwa timu hizo zote zipo
katika ushindani mkali.
Tottenham maarufu kwa jina la Spurs
ina pointi nne katika michezo miwili wakati wapinzani wao, Liverpool wana
pointi tatu na wanahitaji ushindi kwa kuwa katika mchezo uliopita walifungwa,
hivyo pointi tatu za leo zinaweza kuamsha furaha ya timu hiyo ambayo ilipotea
wikiendi iliyopita.
Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp
alichukizwa na wachezaji wake kutofuata maelekezo yake katika mchezo uliopita
na kuahidi kuwa atarekebisha makosa na hivyo mchezo wa leo ndiyo unatakiwa
kuthibitisha hilo japokuwa Spurs ni moja ya timu ngumu.
Wakubwa wengine wa ligi hiyo,
Manchester United watakuwa ugenini kwenye Uwanja wa The KC kuwa wageni wa Hull
City, wakati wakali wa London, Chelsea watakuwa nyumbani kukipiga na Burnley
kwenye Uwanja wa Stamford.
Watford watakuwa nyumbani
kuikaribisha Arsenal huku mabingwa watetezi Leicester City wakiwa wenyeji wa
Swansea City.
Vijana wa Pep Guardiola, Manchester
City nao watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Etihad kuwavaa West Ham.
Post a Comment