KOCHA Mkuu
wa Simba, Joseph Omog, amewatolea uvivu wachezaji wake baada ya kuwaambia kuwa
atakayeleta masihara atajikuta akisugulishwa benchi muda wote.
Akizungumza
na DIMBA jijini jana, Omog alisema malengo yake ni kuhakikisha msimu huu
anatwaa ubingwa hivyo hatakubali kuona mchezaji wake hajitumi halafu aendelee
kumtumia.
“Kwanza
ninachoshukuru ni kwamba tangu niichukue timu wachezaji wangu wananielewa ila
lazima niseme atakayekwenda tofauti hasa kwenye suala la kujituma hatapata
namba.
“Nadhani
hili lipo duniani kote kwamba yule mchezaji ambaye hajitumi mazoezini muda
mwingi hukaa benchi japo si mara zote kwamba anayeanzia benchi ni mbaya,
inategemea na kikosi kilichopo,” alisema.
Alisema yeye
ni muumini wa kuwapa wachezaji wote nafasi ili kuonyesha uwezo wao na
ataendelea kufanya hivyo kadiri ligi inavyokwenda ila akatoa tahadhari kwa
wachezaji hao kukaza buti.
Omog ana
kibarua kigumu cha kuhakikisha kikosi chake kinatwaa ubingwa msimu huu baada ya
Wekundu hao wa Msimbazi kushindwa kufanya hivyo kwa misimu minne mfululizo
wakiwaachia wapinzani wao Yanga pamoja na Azam FC kubadilishana nafasi za juu.
Post a Comment