salvatory kushoto |
Na Mwandishi
Wetu
KIUNGO wa
zamani wa timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Ngawina
Ngawina, pamoja na kiungo wa zamani wa Yanga, Salvatory Edward wameanzisha
kituo cha kuibua vipaji vya wanasoka chipukizi chini ya umri wa miaka 17 na
kuviendeleza.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Ngawina alisema kituo chao kinaitwa Kambiasso Sports na
kwamba kwa kuanzia Jumamosi wiki hii watafanya kliniki maalum ya kusaka vipaji
hivyo kwenye Uwanja wa Tandika Mabatini, Dar es Salaam, dhamira yao kubwa ikiwa
ni kuhakikisha wachezaji wenye vipaji wanaendelezwa na kutafutiwa timu.
“Kila mzazi
mwenye mtoto ambaye anaamini ana kipaji cha soka na anahitaji aendelezwe,
amlete mwanae Tandika Mabatini Jumamosi Agosti 27, ajitahidi saa mbili asubuhi awe ameshafika,
kwani ndiyo muda tutakaoanza.
“Kliniki
yetu itaendeshwa na makocha mahiri, ambao wana leseni za ukocha kutoka CAF
(Shirikisho la Soka Afrika), ili kufanya hili jambo kiuweledi zaidi na kupata
vijana wenye sifa,” alisema Ngawina.
Alisema
dhamira yao ni kupata vijana wengi wenye vipaji kadri iwezekanavyo na kwamba
suala la idadi itategemea na watakavyoona siku hiyo, lakini dhamira yao ni kuwa
na vijana wasiopungua 30, lakini si lazima wote wapatikane Dar es Salaam,
wataenda hadi mikoani.
....akiwa na Marcio MAximo |
Aliwataja
watakaoendesha mshujo huo licha ya yeye na Salvatory, pia atakuwepo kocha
Kennedy Mwaisabula, ambaye amepata kufundisha timu mbalimbali nchini ikiwemo
Yanga.
Mwingine ni
kipa wa zamani wa timu mbalimbali ikiwemo Simba ya Dar es Salaam na Ferroviario
De Maputo ya Msumbiji, Muharami Mohammed ‘Shilton’, ambaye kwa sasa ni kocha wa
makipa wa timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ .
Pia atakuwepo kocha mwingine wa makipa Terry Muhorel.
“Soka si
kama paa la nyumba kwamba siku zote linakuwa juu tu. Soka inaanzia chini na
ndiko tunakotaka twende,” alisema Ngawina.
Kwa upande
wake Salvatory alisema dhamira yao ni kuwa na kituo ambacho kitakuwa hazina ya
nchi kwa wachezaji wa siku za usoni, lakini pia kiwe kitovu cha timu mbalimbali
kuchukua wachezaji.
“Tunaamini
vijana wetu wakishaiva tutawauza timu mbalimbali za ndani ya Tanzania na nje,
kwani kituo kina uhusiano mzuri na watu mbalimbali waliopo hapa nchini na hata
nje ya nchi,” alisema Salvatory.
“Tunaosimamia jambo hili tumecheza mpira kwa
kiasi cha kutosha, tumesomea ukocha, tunajua nini cha kufanya kuendeleza vijana
wetu,” alisema.
Aliwaomba
wachezaji chipukizi wa umri huo wanaoamini wana uwezo wajitokeze siku hiyo ili
kuwania nafasi ya kuwepo katika kituo hicho ambacho kitakuwa Temeke, Dar es
Salaam.
Post a Comment