KOCHA Msaidizi wa Simba,  Jackson Mayanja, amesema JKT Ruvu, inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa ni noma,  kwani  si timu ya kuidharau katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Mayanja amesema kikosi hicho kimeonekana kujipanga msimu huu tofauti na ule uliopita, baada ya juzi kutoka suluhu katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijni Dar es Salaam.
Alisema kuwa mfumo walioingia nao uwanjani JKT Ruvu ilikuwa ni vigumu kwao kupata matokeo ya ushindi,  licha ya mara kwa mara kufika langoni mwao.
“Mchezo ulikuwa mgumu, kwani tulijaribu kufunga,  lakini bahati haikuwa upande wetu, na hii imetokana na jinsi walivyojipanga JKT Ruvu na  inaonyesha kuwa ligi ya msimu huu si rahisi,” alisema.
“Matokeo haya tuliyoyapata yanatupa mwanga vipi ligi ilivyo na hivyo tunatakiwa kujipanga ili kutoruhusu makosa yaliyojitokeza yasiweze kutokea tena, lakini mipango yetu msimu huu ni kuona tunapata ushindi katika kila mechi,” alisema.
Kwa matokeo hayo, Simba wanashika nafasi ya pili wakiwa na pointi nne, sawa na Azam wanaoongoza katika msimamo wa ligi hiyo, lakini wakitofautiana mabao ya kushinda na kufungwa.

Post a Comment

 
Top