Kumbe Majabvi ni bonge la tajiri
NA SAADA SALIM
JUSTICE Majabvi si jina geni masikioni mwa wadau wa soka, hasa mashabiki wa soka hapa nchini. Aliwahi kuwa beki mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo wa Simba na kucheza kwa kiwango kizuri katika kikosi cha Simba kwa msimu uliopita.
Ukimuona jamaa nje na ndani ya uwanja anaonekana wa kawaida sana, hana majivuno wala makuu akiwa katika kazi na hata nje ya kazi yake.
Ni mpole na mtulivu, lakini ni mtu mwenye uwezo mkubwa ndani na nje ya uwanja. Ndani ya uwanja uwezo wake unajulikana kwa kazi aliyofanya akiwa na kikosi cha Simba msimu wa mwaka jana.
Lakini ukija nje ya uwanja, jamaa ni bonge la tajiri mkubwa na staa, pia ni mchezaji anayeheshimika nchini Zimbabwe.
BREAKING NEWS lilipata bahati ya kuzungumza na nyota huyo, lakini baadaye ikapata mkazo kutoka kwa Msemaji wa Simba, Haji Manara.
Maisha ya Majabvi Zimbabwe:
Manara anasema viongozi wa Simba walifanikiwa kufika nchini Zimbabwe na kufikia katika moja ya hoteli zinazomilikiwa na mchezaji huyo.
“Huyu jamaa ni bonge la tajiri nchini kwao, si wa kudharauliwa kabisa, kwani hapa nchini tulikuwa tukimdharau, lakini viongozi wa Simba waliofanikiwa kufika kule walistaajabu utajiri alionao mchezaji,” anasema.
Manara anasema mchezaji huyo anamiliki majumba makubwa na yenye thamani, kuna baadhi ya nyumba amezifanya za biashara ambazo walifikia viongozi wa Simba kwa ajili ya mazungumzo na Kocha Pasuwa.
Magari ya kifahari:
“Kwa utajiri aliokuwa nao, ukiachilia mbali majumba anayomiliki, pia kuna magari ya kifahari anayomiliki, kwani mmoja ya magari yake walikuwa wakitumia viongozi wa Simba, Zacharia Hanspope na mjumbe Collen Frisch alipokuwa nchini Zimbabwe,” anasema.
Manara anasema viongozi hao walipofika nchini humo walipokelewa na mchezaji huyo na kupelekwa katika moja ya hoteli zake na kutoa gari lake la kifahari kwa ajili ya viongozi wake hao kufanyia safari zake za mjini.
Anasema Pope na Collen walikuwa nchini humo kwa ajili ya kufuatilia mchakato wa Kocha Pasuwa ili kuja kuifundisha Simba, lakini ilishindikana baada ya timu ya taifa ya Zimbabwe kufanya vizuri katika michuano ya AFCON.
Kususa nyumba, kuishi hotelini:
Manara amesema kutokana na jinsi ya maisha ya mchezaji huyo yalivyo, alikuwa ana haki ya kuugomea uongozi nyumba ambayo walimpa, kwani ilikuwa haina hadhi na alivyo kwa maisha yake.
“Tulimtafutia nyumba maeneo ya Sinza lakini aliikataa na kudai haiendani naye, hivyo tukalazimika kumpeleka Lamada, moja ya hoteli nzuri ambayo aliridhika kuishi kutokana na kuendana kidogo na mazingira anayoishi nchini Zimbabwe,” anasema Manara.
Majabvi hajarejea tena katika kikosi cha Simba na badala yake alimleta beki mwingine, Method Mwanjali, kuziba nafasi yake, badala ya yeye kwenda nchini Sweden kumalizia soka lake na kumsaidia mke wake anayeishi huko.
Kwa mujibu wa Majabvi mwenyewe, anasema kwamba mpira ndio uliomfanya awe katika maisha aliyonayo sasa. Kwa maana kwamba soka limebadilisha maisha yake na kwamba yeye ni miongoni mwa wanasoka matajiri nchini kwao Zimbabwe.
Post a Comment