SAA chache baada ya kuaga rasmi michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Africa, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga sasa wanaelekeza hasira zao katika Ligi Kuu ili kutetea taji lao linalowaniwa vikali.

Yanga ilikamilisha mchezo wa robo fainali jana dhidi ya TP Mazembe kwa kufungwa mabao 3-1 mjini Lubumbashi na sasa inarejea nyumbani ikipania kuwapoza mashabiki wake kwa kutetea ubingwa huo wa Ligi Kuu.

Kocha Mkuu wa Yanga Hans Van Pluijm, akizungumza mara baada ya mchezo huo alisema, mwisho wa safari yao katika michuano hiyo ndiyo mwanzo wa kujipanga upya kuelekea msimu ujao ambapo kwa sasa akili zao inabidi wazihamishie katika michuano hiyo mikubwa nchini.

“Tumehitimisha safari yetu kwenye Kombe la Shirikisho lakini vita iliyo mbele sasa ni kutetea ubingwa wetu kwenye Ligi Kuu ili kuwapoza mashabiki wetu,”alisema.
Alisema, wanarejea nchini wakiwa na kazi moja tu kutetea ubingwa wao na kujipanga na michuano mingine iliyo mbele yao.Yanga inatarajia kukipiga na African Lyon Jumapili hii uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam ukiwa ni mchezo wake wa kwanza tangu Ligi Kuu Bara ianze Agosti 20 mwaka huu.

Post a Comment

 
Top