KOCHA Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, amekiri
kuwa bado kuna upungufu kwenye safu yake ya ushambuliaji ambayo amepanga
kuiimarisha ili wapate ushindi wa mabao mengi kwenye Ligi Kuu Bara.
Safu ya ushambuliaji ya Simba inaundwa na Mrundi, Laudit Mavugo, Muivory
Coast Fredric Blagnon, Ibrahim Ajib na Daniel Lyanga.
Tatizo hilo la ushambuliaji, pia Kocha Mkuu wa Yanga Mholanzi, Hans
Pluijm amekuwa akililalamikia kutokana na washambuliaji wake, Amissi Tambwe,
Donald Ngoma na Obrey Chirwa kushindwa kutumia nafasi nyingi wanazozipata
kwenye mechi.
Akizungumza na Championi
Jumamosi, Omog alisema idara zote zimekamilika kwenye kikosi chake huku
akitaja safu ya ushambuliaji ndiyo yenye upungufu inayohitaji kuboreshwa.
Omog alisema, tatizo hilo ameliona kwenye mechi ya ligi kuu dhidi ya
Ndanda FC wiki iliyopita ambayo kama washambuliaji wake wangekuwa makini, basi
wangefunga mabao zaidi ya matano.
Aliongeza kuwa, baada ya kugundua upungufu huo, tayari amewapa mbinu
mbalimbali za kufunga mabao ikiwemo mashuti ya mita 20 na kumchambua kipa.
“Kikosi changu kipo fiti kila sehemu, lakini tatizo lililopo ni kwenye
safu ya ushambuliaji ambayo inahitaji uboreshaji mdogo ili kuhakikisha timu
inapata ushindi wa mabao mengi.
“Uzuri, upungufu huo nimeuona mapema na tayari nimeanza kuufanyia baadhi
ya marekebisho kuhakikisha washambuliaji wangu wanafunga kila nafasi
tutakayoitengeza.
“Kikubwa ninataka washambuliaji wangu wacheze kwa nidhamu kubwa na
kutimiza majukumu yao ya kufunga na kutengenezeana nafasi za kufunga,” alisema
Omog.
Post a Comment